Utangulizi
Mifugo ni rasilimali ambayo huwapa faida kubwa wafugaji na wananchi kwa ujumla. Ili mifugo itoe mazao yenye tija inahitaji kupatiwa huduma bora za malisho, maji, kinga na tiba za maradhi. Maradhi ni moja kati ya matatatizo yanayozorotesha sekta ya ufugaji na kupunguza uzalishaji. Katika kukabiliana na changamoto hiyo hatua za kuyadhibiti maradhi zinachukuliwa duniani kote ili kuimarisha ufugaji na kupata tija.
Chanjo
Chanjo ni mchanganyiko maalum wenye vijidudu ambavyo vimepunguzwa nguvu ili visilete madhara kwa wanyama au watu waliochanjwa. Hii ni njia mojawapo inayotumika katika kudhibiti maradhi duniani. Asili ya chanjo ilitokana na ugunduzi wa mwanasayansi wa Uingereza Bw. Edward Jenner katika karne ya 18 ambapo aligundua kwamba wahudumu wa ng’ombe hawakupata ugonjwa aina ya ndui (small pox) kutokana na kuwa na vijidudu vya ugonjwa wa ndui za ng’ombe (cow pox) hali ya kuwa maeneo mengine wasiokuwa wahudumu wa ng’ombe waligundulika kuwa na ugonjwa huo.
Chanjo husababisha mwili wa mnyama au binadamu kuandaa askari (vikinga mwili ni antibody) ambao hukaa mwilini kwa muda maalum na huukinga mwili kukabiliana na vijidudu vya maradhi. Aidha, chanjo ikipungua nguvu inahitajika wanyama wachanjwe tena kwa muda maalum uliopendekezwa kutokana na aina ya chanjo au mnyama.
Aina za chanjo
Miongoni mwa chanjo maarufu zinazotumika kwa mifugo ni; Hitcher B1, LaSota, S19/ Rev- 1 strain, Blanthrax, Rabisin, Tetanus Toxoid, Newcastle Disease vaccine EDS – 76 + ND + IBD, Fowl pox, Clon CL/76 strain, Canine distemper, Marek’s disease vaccine, Foot and Mouth Disease, Gumboro, Mahepe/Mdondo/Kideri, Ndui, Pepopunda, Kimeta, Chambavu, Ugonjwa wa kutupa mimba kwa ng’ombe, Ugonjwa wa mapafu wa ng’ombe na mbuzi, Ugonjwa wa bonde la ufa, Ugonjwa wa ngozi (Lumpy skin, Streptothricosis, Warts, Mange) Ugonjwa wa miguu na midomo,
Maradhi yanayochanjwa na muda unaopendekezwa
- Chanjo ya Gumboro kwa kuku wachanga mara moja katika uhai wake
- Chanjo ya Mahepe/Mdondo/Kideri kwa kuku mara mbili katika uhai wake
- Chanjo ya Ndui kwa kuku na ng’ombe mara moja;
- Chanjo ya ugonjwa wa kutupa mimba kwa ng’ombe mara moja kwa mwaka
- Chanjo ya ugonjwa wa Kimeta kwa ng’ombe kila mwaka;
- Chanjo ya ugonjwa wa Chambavu kwa ng’ombe kila mwaka;
- Chanjo ya ugonjwa wa pepopunda (Tetenasi ) kwa ng’ombe kila mwaka
- Chanjo ya ugonjwa wa ngozi kwa ng’ombe, mbuzi na kondoo kila mwaka
- Chanjo ya ugonjwa wa miguu na midomo kwa ng’ombe kila mwaka;
- Chanjo ya ugonjwa wa homa ya mapafu kwa ng’ombe na mbuzi kila mwaka
- Chanjo ya Kichaa cha mbwa kwa mbwa kila mwaka;
- Chanjo ya ugonjwa wa matumbo hasa kwa mbwa wadogo pia unaweza kuchanja kwa wakubwa kila mwaka
- Chanjo ya Ugonjwa wa sotoka kwa ng’ombe kila mwaka
- Chanjo ya ugonjwa wa bonde la Ufa kwa ng’ombe;
- Chanjo ya ugonjwa wa Farasi kwa farasi kila mwaka.
Wanyama wanaochanjwa
Wanyama hao ni pamoja na ng’ombe, mbuzi kondoo, nyati, ngamia, mbwa, paka, farasi na jamii ya ndege wakiwemo kuku wa aina zote wa mayai nyama na wa kienyeji.
Faida za Chanjo
- Chanjo hudhibiti magonjwa yanayosababishwa na vimelea vya aina ya virusi, bektiria, rikesia na protozoa;
- Chanjo huongeza uwezo wa mnyama kujikinga na maradhi;
- Chanjo hulinda afya ya mifugo baada ya lishe bora na;
- Chanjo hudhibiti magonjwa yasiyoweza kutibika.
Njia na sehemu za kuchanja
- Kupitia mdomoni kwa magonjwa ya mahepe/mdondo/kideri, Gumboro kwa kuku;
- Kwenye bawa kwa ugonjwa wa ndui kwa kuku;
- Chini ya ngozi kwa magonjwa kama ya ngozi.
Mambo ya kuzingatia katika uchanjaji
- Chanjo zihifadhiwe kwenye hali ya ubaridi na zisiwekwe kwenye joto au mwanga wa jua, wanyama wanaochanjwa ni lazima wawe na afya nzuri na hawajaambukizwa magonjwa yaliyokusudiwa kuchanjwa. Inashauriwa chanjo zifanywe na wataalamu wa mifugo au wafugaji waliopewa mafunzo ya kuchanja.
- Chanjo zinaweza kuleta madhara ikiwa zitatumiwa wakati muda wake wa matumizi umekwisha (expired).
- Aidha, chanjo zenye vijidudu vilivyohai zinaweza kuambukiza maradhi kwa wanyama waliochanjwa.
Comments
Post a Comment