Utunzaji Bora wa Kuku wa Kienyeji
Kuku wa kienyeji ni wale wa kiasili ambao hufugwa zaidi vijijini na wananchi ambao ni zaidi ya asilimia 80 ya idadi ya Watanzania wote. Kwa kawaida kuku hawa hujitafutia chakula chao wenyewe na wana uwezo wa kustahimili mazingira magumu. Vile vile wana uwezo wa kuatamia mayai na kutotoa vifaranga. Asilimia kubwa ya mayai na nyama inayotumika vijijini hutokana na kuku hawa na hata hivyo nyama na mayai yanayozalishwa ni kidogo kutokana na utaalamu duni. Ili kuongeza kiwango cha uzalishaji ni muhimu kufuata kanuni za ufugaji bora kama vile, banda bora, uchaguzi wa kuku walio bora, uanguaji na uleaji wa vifaranga, chakula bora na kuzuia magonjwa.
Banda Bora
Kuku wa kienyeji wanahitaji mahali safi na bora pa kulala. Kwa hiyo ni muhimu kuwajengea banda ambalo linaingiza hewa na mwanga wa kutosha. Banda liwe rahisi kusafishwa, na eneo la kutosha kufuatana na idadi ya kuku. Inafaa kuwawekea nyasi kavu au makapi ya mazao sakafuni. Eneo la kufugia lizungushiwe uzio.
Uchaguzi wa Kuku Bora
Chagua kuku mwenye sifa zifuatazo:
- Wenye kukua haraka.
- Wenye uwezo wa kustahimili magonjwa, wanaotaga mayai mengi.
- Wawe na uwezo wa kuatamia na kuangua vifaranga wengi na kuwalea.
Pamoja na sifa hizo, katika kundi la majogoo uchague aliye na umbile zuri, mkubwa, uzito wa wastani, mwenye rangi ya kuvutia na pia awe na kucha fupi. Kama huna kuku wenye sifa hizo, unashauriwa kuwanunua kutoka mahali pengine. Unashauriwa uwiano wa majogoo na majike uwe moja kwa kumi.
Uanguaji wa Asili wa Vifaranga
Huu ni uanguaji unaofanywa na kuku kwa kuatamia mayai. Kwa kawaida kuku mmoja anaweza kuatamia mayai 12 hadi 15 kwa mara moja. Kuku awekewe mayai ya kuanguliwa wakati wa kuatamia ukifika. Unashauriwa kumwekea kuku mayai ya kuatamia wakati wa usiku na sio mchana kwa sababu kama atawekewa wakati wa mchana anaweza kuyaacha.
Matayarisho ya Kiota
Kiota kitayarishwe kabla kuku hajaanza kutaga. Kama kiota kitawekwa chini, sehemu ya kitako iwekewe wavu wa chuma wenye matundu madogo ya sentimita moja na robo. Wavu huu unasaidia kuzuia wanyama waharibifu kama vile panya. Ndani ya kiota ziwekwe nyasi kavu na zisambazwe mfano wa kisahani. Kiota kiwe safi na kinyunyiziwe dawa ya unga ya kuua vijidudu kabla ya kuweka nyasi. Kila baada ya kuangua, kiota kisafishwe. Endapo kuku atajitengenezea kiota chake mwenyewe ambacho kipo mahali panapofaa na penye usalama, inafaa aachiwe kiota hicho.
Kumtayarisha Kuku wa Kuatamia
Kuku wanaotazamiwa kuatamia ni lazima wachunguzwe kwa makini siku mbili kabla ya kuatamia ili kuhakikisha kwamba hawana chawa, utitiri au viroboto. Kuwepo kwa wadudu hao huwafanya kuku wakose raha na wasitulie kwenye viota vyao. Hali hii husababisha kuanguliwa kwa vifaranga wachache. Ikiwa kuku wana wadudu hao wanyunyizie dawa. Kwa ushauri zaidi muone mtaalamu wa mifugo.
Kuku kwa ajili ya kuatamia awe na tabia na uwezo wa kuatamia na kuangua vifaranga wengi.
Kuchagua Mayai ya Kuangua
Mayai yanayofaa kuanguliwa yawe na ukubwa wa wastani, yasiwe na nyufa, yasiwe ya mviringo kama mpira, yasiwe na uchafu wowote juu ya maganda na yasiwe yametengwa zaidi ya juma moja.
Mayai yanayofaa ni yale yaliyotagwa na kuku aliyepandwa na jogoo.
Uanguaji
Uanguaji wa vifaranga huchukua siku 21 tangu siku ya kwanza ya kuatamia. Katika juma la tatu ni muhimu sana kwa utotoaji. Kwa hiyo kuku apewe maji na chakula cha kutosha kila siku ili atulie.
Mayai huanza kuanguliwa siku ya ishirini baada ya kuanza kuatamiwa. Mara tu baada ya uanguaji kukamilika, maganda ya mayai na mayai ambayo hayajaanguliwa yaondolewe kwenye kiota na kuchomwa moto.
Kulea Vifaranga
Kuku mwenye vifaranga awekwe mahali penye usalama, kwa muda wa mwezi mmoja au zaidi ili vifaranga wasichukuliwe na mwewe, vicheche, paka, kenge na kadhalika. Wape maji na chakula cha kutosha kwa muda wote Iwapo kuku wengi watakuwa wameangua kwa wakati mmoja, achaguliwe yule mwenye tabia ya kulea vifaranga ili aendelee kulea vifaranga wote na wale kuku wengine warudi katika utagaji. Kwa kufanya hivyo mfugaji ataweza kuzalisha kuku wengi kwa muda mfupi Vifaranga wapatiwe chanjo dhidi ya magonjwa mbali mbali kama vile Mdondo, Mahepe na Gumboro. Vile vile wapatiwe dawa za kuzuia minyoo. Kuku wanaokua waendelee kupewa maji na chakula cha ziada kila siku, chanjo na dawa za kuzuia minyoo.
Comments
Post a Comment