Utangulizi
Kitalu ni sehemu maalumu iliyopangiliwa kwa ajili ya kutunzia miche michanga kabla ya kuipeleka shambani ama bustanini. Sio mimea yote inahitaji vitalu ila mimea mingi inahitaji vitalu. Mimea kama mahindi, maharage, karoti, kunde na mchicha haihitaji vitalu. Mimea kama kabeji, vitunguu, sukuma wiki, chainizi, nyanya, bilinganya, hoho, matikiti, matango na mengineyo huhitaji kitalu. Pia miti mingi ya matunda, kuhifadhi mazingira, mbao, dawa nakadhalika huhitaji kitalu. Mimea ambayo inasumbua kupandikiza na ambayo inachipua haraka inashauriwa kupandwa moja kwa moja shambani ambapo haitasumbuliwa kuhamishwa. Mimea ambayo inachelewa kuchipua, kukua, na yenye kuhitaji matunzo au kuhudumiwa kwa karibu wakati ikiwa michanga inashauriwa ipandwe kwanza kwenye kitalu hadi itakapopata miche inayotakiwa kisha kupandikizwa bustanini au shambani.
Aina za vitalu
- Vitalu vya kawaida vya matuta
- Vitalu vya vimfuko (viriba)
- Vitalu vya boksi
Namna ya kuchanganya na upandaji
Weka udongo debe mbili, mbolea debe moja na makapi ya mpunga ama mchanga debe moja. Changanya vizuri kwa kutumia koleo na utandaze huo mchanganyiko kwa kutumiaa reki. Panda au sia mbegu bora ambazo zimekomaa na kukauka vizuri, ambazo hazijashambuliwa na magonjwa au wadudu na zenye uwezo wa kuota vizuri zikipandwa. Kama unahitaji kununua mbegu inashauriwa kununua mbegu kutoka kwa mawakala wanaoaminika. Unaweza kupanda kwa mstari ama kwa kusia. Miche ikiwa tayari ikapandwe bustanini wakati wa jioni na imwagiliwe vizuri. Bustani iwe imeandaliwa kabla ya siku ya kuhamisha miche. Udongo kwenye kitalu unatakiwa uwe unaweza kupitisha maji vizuri. Tayarisha kitalu chako kwa kuchimba au kulima udongo angalau 30 sm kwenda chini, ondoa mabaki yoyote ya mimea na mizizi na vunja mabonge yote ya udongo kisha changanya samadi iliyooza vizuri au mboji iliyoiva vizuri. Sawazisha vizuri na reki hadi udongo uwe vizuri.
Pima upana na urefu wa kitalu ambao utakuwezesha kufikia kila pembe ya kitalu kwa urahisi bila kukanyaga ndani ya kitalu. Hii itasaidia kupunguza uwezekano wa kuleta magonjwa kwenye kitalu na itarahisisha kungoa magugu pamoja na kuhamisha miche kwenda shambani. Kama unasia mbegu katika mistari hakikisha kuwa mistari ipo katika umbali wa sm 7-10. Baada ya kusia mbegu funikia na udongo kidogo kutegemea na ukubwa wa mbegu. Siku moja kabla ya kusia mbegu, mwagia kitalu maji hadi kilowe vizuri. Kwa siku zinazofuata inashauriwa kumwagilia maji kidogo kidogo hadi pale zitakapochipua.
Namna ya kutayarisha kitalu
Mahitaji
- Makapi ya Mpunga
- Debe
- Mbolea samadi au mboji
- Jembe au Koleo
- Udongo
- Maji na Reki
Sifa za sehemu nzuri ya kutengeneza kitalu
- Karibu na chanzo cha maji au bomba.
- Sio mbali na shambani/bustanini.
- Mbali na wanyama ama kuwe na uzio.
- Pasiwe na upepo mkali
- Iwe na kivuli.
- Iwe karibu na njia kurahisisha usafirishaji pindi ikibidi.
Matunzo ya kitalu
Baada ya kusia mbegu hakikisha kitalu hakipati jua la moja kwa moja na mvua kubwa. Weka matandazo ya majani ili kusaidia udongo kuhifadhi unyevunyevu na kuweza kuzuia mwangaza wa jua wa moja kwa moja.
Angalizo:
- Ondoa matandazo mara tu mbegu zitakapochipua
- Ruhusu kivuli kidogo kwenye miche na usiweke kivuli kikubwa sana kwani kitaifaya miche isikue
- Baada ya kuchipua mwagilia maji taratibu kwa kutumia bomba au chupa yenye vitundu vidogo dogo.
- Hakikisha maji hayazidi kwenye kitalu kwani yanaweza kusababisha ugonjwa na miche kuharibika.
- Hakikisha kitalu ni kisafi wakati wote. Ondoa magugu yoyote yatakayojitokeza.
- Punguzia miche kama imejazana sana ili kuipa nafasi ya kukua vizuri.
- Kagua kitalu mara kwa mara kuangalia kama kuna uvamizi wowote wa wadudu waharibifu au mlipuko wa ugonjwa.
Baada ya miche yako kufikia muda wa kupandikiza inashauriwa kuchagua miche yenye afya nzuri ambayo haijaathirika na wadudu wala kuwa na dalili yoyote ya ugonjwa. Mwagilia maji kwenye kitalu usiku mmoja kabla ya siku ya kung’oa ili kurahisiha ung’oaji na kuzuia uwezekano wa mizizi kuharibika. Hakikisha miche iliyong’olewa haipati jua la moja kwa moja au hewa yenye joto. Inashauriwa kuiweka kwenye trei au kikapu na kuifunika na majani au nguo mbichi wakati inapelekwa shambani au bustanini.
Namna ya kupandikiza miche kwenye Shambani/Bustanini
- Panga kupandikiza miche shambani au bustanini siku ambayo jua siyo kali sana au wakati wa jioni wakati jua linakaribia kuzama.
- Manyunyu ya mvua ni muhimu na husaidia sana wakati wa kupandikiza.
- Shindilia udongo vizuri kuzunguka mizizi ya mche kwa kutumia vidole vyako ili kuufanya mche ujishike vizuri kwenye udongo.
- Hakikisha unaweka nafasi ya kutosha kati ya mmea na mmea na mstari hadi mstari ili kuacha nafasi ya mizizi kutanukia na majani kuchanulia hapo baadaye.
- Kama hamna mvua wakati wa kupandikiza inashauriwa kumwagilia hata kama mimea haionyeshi dalili za kukauka.
- Ikinge mimea iliyopandikizwa na jua la moja kwa moja hadi wakati ambapo itaonyesha kuwa imeshika kwenye udongo, inaweza kukua yenyewe na kuhimili mwanga wa jua.
Faida za Kitalu cha miche kwa mkulima
- Kuchagua miche iliyo na afya nzuri.
- Kuthibiti magugu shambani kabla hajahamishia miche shambani.
- Kupata miche ya kupanda muda wowote atakao.
- Ni rahisi kuthibiti vijidudu viharibifu na magonjwa kwenye kitalu kuliko shambani ama bustanini. Hii ni kwa sababu kitalu kinakua na miche mingi na huchukua nafasi kidogo.
- Ni rahisi kuhudumia miche iliyo kwenye kitalu kuliko bustanini.
- Kuweza kuuza miche kwa wakulima wengine.
Comments
Post a Comment