Skip to main content

Kilimo cha Mboga, Matunda Kinavyoweza Kukuza Uchumi


KILIMO ni kilimo tu iwe mjini au vijijini ilimradi kimnufaishe mkulima na kupata faida kwa kile alichoamua kuzalisha.

Makala haya yanajikita kwenye kilimo ambacho wengi wanaweza kushangaa kwa sababu ya asili ya kilimo chenyewe. Ukitaja neno kilimo wengi hukifikiria kilimo cha mashambani hasa vijijini. Kilimo ninachokizungumzia ni cha mboga zikiwemo hoho, nyanya, biringanya, vitunguu, kabeji, matembele na mchicha. Kilimo hiki kinaweza kufanyika katika njia kuu mbili: kwanza ni kwa kutumia njia ijulikanayo kama ‘green house’ na kilimo cha wazi ambacho hufanyika katika maeneo maalumu ya wazi ambayo serikali inatakiwa iyaweke inapopanga mipangilio ya miji.

Katika kufahamu undani wa kilimo hiki, mwandishi wa makala haya amefanya mahojiano na Mtaalamu wa Mipango Miji na Mhadhiri Msaidizi kutoka Chuo Kikuu cha Ardhi, Hussein Kayera. Kwanza anaeleza historia ya kilimo hiki cha mboga mijini Tanzania na namna wananchi wanavyoweza kunufaika na shughuli hizo. Kayera anasema, kilimo cha mboga mijini kipo kwa mujibu wa sheria lakini hakuna maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya shughuli hizo.

Kwa mujibu wa Kayera, kilimo cha mboga mijini kiliruhusiwa rasmi na serikali mwaka 1970 na kuzuiliwa mwaka 1980 kabla ya kurejeshwa tena rasmi mwaka 2000. Anasema, kilimo hicho kinaweza kuzalisha mboga kama vile nyanya, biringanya, hoho, mchicha, matembele na nyanya chungu.

“Kilimo cha mboga mijini ni kizuri sana na pia kipo kwa mujibu wa sheria lakini serikali ndiyo imeshindwa kutenga maeneo maalumu kwa ajili ya shughuli hizo za kilimo” “Serikali ilitakiwa itenge maeneo tangu mwaka 2000 ilipopitisha sheria ya kutambua kilimo cha mijini, lakini hakuna juhudi zozote zilizofanyika na badala yake wananchi wanajilimia kando kando ya mito na mifereji ya maji machafu yanayotoka viwandani ambayo huhatarisha afya,” anasema Kayera.

Kayera anasema, kilimo hicho kinakabiliwa na changamoto kadhaa ukiwemo ukosefu wa maeneo maalumu yaliyotengwa na serikali kwa ajili ya kufanyia shughuli hizo za uzalishaji wa mboga. Anataja changamoto nyingine kuwa ni kutokuwa na uhakika wa kumiliki eneo mijini kwa ajili ya kilimo na pia wakulima wanatumia maji machafu ambayo ni hatari kiafya. Anasema, baadhi ya wakulima wa kilimo hicho mijini hutumia viuatilifu bila ya kufuata taratibu, kitu ambacho husababisha madhara makubwa kiafya.

Kayera anasema, utumiaji wa ardhi na maji yasiyokuwa salama unaweza kusababisha uzalishaji wa mazao yasiyokuwa salama na hivyo huhatarisha afya za walaji. Changamoto nyingine inayotajwa kuwakabili wakulima wa mboga mijini ni ukosefu wa soko la kimataifa na ugumu wa hifadhi za mboga ili zikae muda mrefu bila kuharibika. Kayera anasema, kilimo hicho kikipewa kipaumbele kitasaidia kupunguza tatizo la ajira, kitaongeza uzalishaji wa mboga bora ambazo hazina kemikali ukilinganisha na zile zinazozalishwa kwenye mifereji ya maji machafu yatokayo viwandani.

Mkulima wa mboga katika eneo la Msimbazi jijini Dar es Salaam, Janeth Mlinga, anasema kilimo hicho ndicho kinachoendesha maisha yake. Kwa muda mrefu, kumekuwa na tuhuma kwamba, mboga zinazozalishwa katika bonde la mto Msimbazi ni hatari kwa afya kwa muwa wakulima wanatumia maji yenye kemikali yanayotoka viwandani.

“Kilimo hiki ni kizuri sana kwani ndio msingi wa maisha ya familia yangu, napata hapa chakula na mahitaji ya kila siku ya familia yangu japokuwa wengi yanasema kuwa mboga zinazozalishwa hapa ni mbaya na zina madhara kwa afya, hii sio kweli kwani sijasikia mtu aliyekufa kwa kula mboga zilizozalishwa katika bonde hili,” anasema Mlinga. Inadaiwa kuwa, kama wananchi wengi wa mkoa wa Dar es Salaam wangekuwa wanatembelea maeneo zinapozalishwa mbogamboga wanazokula wangeendelea kuzila kwa sababu zinalimwa kwenye mazingira machafu, na maji yanayotumika kumwagilia pia yanakatisha tamaa.

Mlinga anasema, yeye ameanza kulima mchicha, matembele na bamia katika bonde hilo kwa miaka zaidi ya 10 sasa na hajawahi kupata kesi wala kusikia kutoka hospitalini kuwa kuna mtu amefariki dunia kutokana na kutumia mboga zilizotoka bonde la Msimbazi. “Mboga tunazozalisha sisi hapa ni nzuri kiafya na pia hata wenyewe tunakula, hivyo kama tunazalisha chakula ambacho hata sisi wenyewe tunatumia, ujue tunazailisha kitu chenye ubora,” anasema Mlinga.

Utafiti uliofanywa na Chuo Kikuu cha Ardhi katika bonde la mto Msimbazi ukijumuisha udongo na maji katika bonde hilo kwa kuzingatia vigezo vya Shirika la Afya dunia WHO na Shirika la viwango nchini TBS, umebaini uwepo wa kemikali na sumu. Utafiti huo uligundua kuwa maeneo mengine yanayotumika kwa ajili ya kilimo cha mbogamboga hutumika kwa kutupia takataka zikiwemo betri zilizoisha muda wa matumizi, masalia ya simu za mkononi, vipuri vya magari na majokofu mabovu.

Taka hizo zenye sumu hutupwa kwenye mifereji ya maji yanayotumika kwa umwagiliaji wa mboga na hivyo kuhatarisha afya za walaji. Katika utafiti huo, imebainika kuwa mboga zinazomwagiliwa na maji yenye sumu pamoja na kemikali yakiwemo madini ya risasi, shaba na kromiamu ni hatari kwa afya ya binadamu.

Utafiti huo unaonesha kuwa mboga zinazozalishwa katika bonde la Msimbazi huuzwa katika masoko ya Ilala, Kariakoo, Buguruni, Veterani, Tazara, Mwananyamala, Mnyamani, Kigogo, Kisutu, Vingunguti, Tabata, Mikoroshini na maeneo ya jirani na wakulima hao mkoani Dar es Salaam.

IMEANDIKWA NA EMMANUEL GHULA - HABARILEO

Comments

Popular posts from this blog

Utengenezaji wa Chakula cha Kuku wa Nyama (Bloilers)

Utangulizi Kuku wa nyama wana mahitaji yafuatayo ya viinilishe katika chakula ili wakue vizuri Viinilisha vya wanga 60-65%   Protini 30-35%   Madini 2-8% Chakula cha Vifaranga Chakula hiki hutengenezwa katika namna ya kumsaidia kifaranga aweze kumeza vizuri na hivyo hakitakiwi kuwa katika punje punje. Hata kama utanunua pumba, ni vema kuzipitisha kwenye mashine ili ziwe laini zaidi.  Mahitaji (kgs)  Unga wa dona wa nafaka kama mahindi au mtama 40  Pumba za mtama au mahindi au uwele 27  Mashudu ya alizeti au ufuta, au pamba au karanga n.k. 20  Unga wa mifupa au chokaa ya kuku (DCP) 2.25  Dagaa au mabaki ya samaki (sangara fish meal) 10  Chumvi ya jikoni 0.5  Virutubisho (Broiler premix) 0.25  Jumla utapata 100Kg. Chakula cha kukuzia – growers mash Mahitaji (Kg) Mahindi yaliyobarazwa au mtama au uwele 25   Pumba za mtama au mahindi au uwele 44   Mashudu ya alizeti au ufuta, au pamba au karanga n.k. 17   Unga wa mifupa au chokaa ya kuku (DCP) 3.25   Dagaa au mabaki ya samaki (fish meal) 1

Aina Za Miti ya Minazi

AINA ZA MINAZI Inafaa mkulima kufahamu kuna aina mbali mbali za minazi na ina mahitaji tofauti katika ukuaji. Ujuzi huu utamsaidia katika kuchagua aina ya minazi itakayofaa kwa eneo lake na kwa kiwango chake cha utunzaji. KUNA AINA TATU ZA MINAZI Minazi mirefu ya asili Minazi mifupi Minazi chotara MINAZI MIREFU YA ASILI (EAT) Minazi ya aina hii ndiyo inayojulikana na wakulima wengi kwa vile ni ya kiasili na imezoea mazingira yetu. Minazi hii huchukua miaka 6-8 tangu kupandikizwa hadi kuzaa. Minazi ya aina hii huvumilia ukame na inao uwezo wa kutoa wastani wa nazi 40 kwa mwaka. Nazi huwa kubwa na zenye nyama nene ambayo inafaa kwa kupikia na kukamua mafuta. Minazi hii huishi kad ya miaka 60 na kuendelea. Nchini Tanzania, minazi hii hustawi vyema ukanda wa pwani sehemu zisizo na mawe na ambazo hazituamishi maji. MINAZI MIFUPI (DWARF) Minazi ya aina hii huzaa mapema kuanzia miaka miwili. Huzaa nazi nyingi na ndogo. Nazi hizi huwa na nyama nyembamba hivyo hutumika kwa nnadafu. Minazi huhit

Kilimo cha Miti ya Mbao - Uwekezaji wa Muda wa Kati na Mrefu

Utangulizi Kilimo cha miti ni uwekezaji wa muda wa kati na mrefu (mid & long term investments). Ila kwa kawaida jamii nyingi hasa za kiafrika huwa hazivutiwi na uwekezaji wa muda mrefu. Hata hivyo kama una mpango wa kuwa imara kiuchumi inashauriwaau yakupasa kufikiria na kujifunza aina za uwekezaji wa muda mrefu. Miti hutumika kwa matumizi mengi mfano mbao, nguzo za umeme na kujengea, mapambo, kuni na mkaa, kuzalisha matunda, mitishamba na madawa,  utengenezeaji wa karatasi n.k.  Mchanganuo Ekari moja ya shamba unaweza kupanda miti mia sita (500) mpaka mia saba (700). Gharama za kununua mashamba au maeneo ya kupandia miti hutegemea na eneo. Kwa  sehemu nyingi za vijijini maeneo kwa ekari moja hayazidi laki 5.  Miche ya kununua mfano Mitiki huuzwa kuanzia elfu moja (1000) kwa mche mmoja Gharama ya kununua miche =  1000 * 600 = 600,000   Pia unaweza kuokoa gharama za kununua miche kwa kuioteshe mwenyewe ktk vitalu na kuiamishia shambani baada ya kustawi vizuri na kuwa imara.  Mf. Mbe