Utangulizi
Mihogo hulimwa kwa wingi katika mikoa ya Mara, Mwanza, Kigoma, Mtwara, Lindi, Pwani, Ruvuna, Tanga, Morogoro, Mbeya, na Shinyanga. Muhogo una kiwango kikubwa cha wanga ukilinganisha na nafaka (zaidi ya asilimia 40 kuliko mchele, na zaidi ya asilimia 25 kuliko mahindi). Majani yake hutumika kama mboga na yana virutubishi muhimu hususan vitamini B na protini.
Uzalishaji wake ni wastani wa tani 1,292,000 kwa mwaka. Ili kupata mazao mengi na bora ni muhimu kuzingatia kanuni za kilimo bora cha mihogo hasa zifuatazo:
Mambo Muhimu ya Kuzingatia Katika Uzalishaji
Kuchagua aina ya mbegu
- Chagua mbegu kufuatana na mahitaji ya soko, zilizo safi zinazostahimili magonjwa, wadudu waharibifu na zenye uwezo wa kutoa mazao mengi na bora.
Palizi
- Palilia ili kupunguza ushindani wa virutubishi kati ya mmea na magugu.
- Palilia na kupandishia udongo kwenye mashina.
- Palizi ifanyike mara kwa mara mpaka mihogo inapokomaa.
Muhogo hushambuliwa na wadudu waharibifu kama vidung’ata, vidugamba, mchwa na magonjwa kama batobato na ugonjwa wa michirizi ya kikahawia. Visumbufu hawa wanaweza kusababisha upotevu wa mazao kwa zaidi ya asilimia 90. Hivyo ni muhimu kukagua shamba mara kwa mara ili kuona kama kuna mashambulizi na kuchukua tahadhari mapema.
Maandalizi kabla ya kuvuna
Kukagua shamba
- Kagua shamba ili kuhakikisha kama muhogo umekomaa. Kwa kawaida muhogo hukomaa katika kipindi cha miezi 9 hadi 24 tangu kupanda kutegemea aina na hali ya hewa. Wakati huo muhogo huwa na unyevu wa asilimia 60 na wanga asilimia 35.
- Udongo unaozunguka shina hupasuka.
- Mti wa muhogo huonekana kupevuka.
- Muhogo uliokomaa ni mnene na ukiutafuna utahisi wanga mwingi na maji kidogo.
vifungashio
Vifaa vya kuvunia na kubeba
- Jembe, Panga, Vikapu, Matenga, na Magunia
- Maboksi ya mbao/plastiki, viroba, Matenga
- Baiskeli, Matoroli, Mikokoteni, Magari na matela ya matrekta.
Ni muhimu kuvuna mapema ili kupunguza uharibifu unaoweza kusababishwa na mashambulizi ya magonjwa na wadudu waharibifu. Kabla ya kuvuna matawi yote yakatwe ili kurahisisha uvunaji.
Njia ya kuvuna muhogo
Chimbua shina la muhogo kwa kutumia jembe na ng’oa muhogo wote kutoka ardhini. Tenganisha muhogo na shina kwa kutumia panga kali.
Utayarishaji, Hifadhi na Usindikaji wa Mazao ya Mizizi baada ya Kuvuna
Tahadhari
Epuka kukata muhogo wakati wa kuvuna kwani mihogo iliyokatwa au kuwa na majeraha huharibika mapema, kutokana na kuingiwa kwa urahisi na vimelea vya magonjwa.
Kuchambua Na Kusafisha
Kuchambua
Lengo la kuchambua ni kuondoa mihogo isiyofaa, iliyooza na iliyokatwa vibaya na kuharibika.
- Mihogo iliyooza isitumike kwa chakula bali ifukiwe.
- Mihogo iliyokatwa au yenye michubuko itumike kwa chakula mapema iwezekanavyo au ioshwe vizuri na isindikwe mara moja.
- Mihogo iliyodumaa itumike kwa chakula cha mifugo.
Kusafisha
Mihogo iliyovunwa huoshwa mara tu baada ya kuvuna ili kuondoa udongo na uchafu mwingine. Mihogo ambayo haikuoshwa vizuri hupunguza ubora wakati wa kukausha na kusindika. Mihogo huoshwa kwa maji na kurudiwa hadi maji yanapokuwa safi na kuona kuwa mihogo imetakata.
Imetolewa na Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika
Comments
Post a Comment