Skip to main content

Kilimo Bora cha Karoti



UTANGULIZI
Karoti ni zao la mizizi ambalo hulimwa zaidi katika mikoa ya Amsha, Kilimanjaro, Morogoro, Iringa, Mbeya na Kagera.
Zao hili hutumika kama kiungo katika mapishi ya vyakula mbalimbali. Huweza kutafunwa mbichi au kuchanganywa kwenye kachumbari. Karoti zina vitamin A, C na madini aina ya chuma.
MAZINGIRA:
Karoti hustawi vizuri kwenye sehemu zenyejoto la wastani (nyuzi joto 15 hadi 27 za Sentigredi).
Kiasi cha mavuno yanayoweza kupatikana na ubora wa karoti, hutegemea sana aina ya udongo. Hivyo karoti hustawi vizuri katika udongo mwepesi, wenye rutuba ya kutosha, kina kirefu na usiotuamisha maji.
AINA:
Kuna aina nyingi za karoti. Zifuatazo ni aina zinazolimwa hapa Tanzania.
  • NantesKaroti za Nantes ni ndefu, huvunjika kwa urahisi, zina umbo la kuchongoka na ncha kali. Aina hii hupendwa sana kutafunwa na walaji, kutokana na ladha yake tamu. Karoti za Nantes hazifai kwa kusindikwa.
  • Chantenay Red CoreHizi ni nene kwa umbo, na zenye ncha butu. Unene wa nyama ya nje na ndani hulingana hivyo zinafaa sana kwa kusindikwa. Huwa na rangi ya machungwa iliyofifia na ladha yake siyo tamu.Aina hii hustawi vizuri kwenye udongo mzito.
  • OxheartKaroti za Oxheart ni fupi na nene. Huvunwa baada ya muda mfupi kulinganisha na aina zingine.
  • Cape MarketAina hii hupendwa sana kutafunwa zikiwa mbichi pia zinafaa kusindikwa.
  • Flacoro
    Aina hii huzaa sana na mizizi yake ni mirefu. Hufaa kwa kuhifadhiwa na kusafirishwa, kwa sababu haziharibiki haraka.
  • Top WeightAina hii ina sifa kama za Flacoro.
 KUTAYAMSHA SHAMBA
Ili kupata mavuno mengi na bora, eneo la kupanda halina budi kutayarishwa vizuri. Iwapo shamba ni jipya, miti na visiki vyote vikatwe. Visiki na takataka zote ziondolewe shambani. Baada ya hapo shamba lilimwe vizuri na katika kina cha kutosha. Lainisha udongo ili kurahisisha uotaji wa mbegu za karoti ambazo ni ndogo sana. Kama eneo lina udongo wa mfinyanzi au wa kichanga ni muhimu kuweka mbolea za asili zilizooza vizuri. Mbolea hizi hufanya udongo wa mfinyazi uwe mwepesi wa kuweza kuruhusu maji na hewa kupenya kwa urahisi. Endapo karoti zitastawishwa wakati wa mvua nyingi zipandwe kwenye matuta yaliyoinuliwa.

KUPANDA
Karoti hupandwa moja kwa moja shambani katika matuta au sesa. Kiasi cha gramu 80 (sawa na vijiko vidogo vya chai 16) kinatosha kupanda eneo la mita mraba 100. Hekta moja huhitaji kilo 8 za mbegu. Hakikisha mbegu unazozipanda zina uwezo wa kuota kwa kuzifikicha. Mbegu zenye uwezo wa kuota hutoa harufu kali unapozifikicha. Zilizopoteza uwezo wa kuota huwa hazitoi harufu yoyote. Ili mbegu ziote haraka ziloweke katika maji kwa muda wa saa 24. Baadaya hapo changanya mbegu hizo na mchanga, kwa kiasi kinacholingana ili kupata mtawanyiko mzuri wa mbegu wakati wa kupanda. Kama utapanda karoti katika matuta, tengeneza matuta yaliyoinuliwa kidogo, kiasi cha sentimita 10 mpaka 15. Matuta haya yawe na upana wa sentimita 60 na urefu wowote. Sia mbegu katika mistari yenye nafasi ya sentimita 30 mpaka 40 kati ya mstari na mstari, na kina cha sentimita moja mpaka moja na nusu. Iwapo utapanda katika sesa tumia nafasi ya sentimita 40 mpaka 50, kati ya mstari na mstari. Nafasi ya kupandia itategemea aina ya karoti inayokusudiwa kustawishwa Baada ya kupanda, weka matandazo kama vile majani makavu na kisha mwagilia maji asubuhi najioni mpaka mbegu zitakapoota. Umwagiliaji utategemea hali ya hewa. Mbegu huota baada ya siku 10 mpaka 15. Zikishaota ondoa matandazo.

KUTUNZA SHAMBA
  • Kumwagilia MajiHakikisha udongo una unyevu wa kutosha hasa siku za mwanzo. Karoti zilizokosa maji kwa muda mrefu huzaa mizizi midogomidogo. Pia udongo mkavu ukipata maji mengi ghafla husababisha karoti kupasuka. Hivyo mwagilia shamba mara kwa mara kuhakikisha udongo una unyevu wa kutosha wakati wote, kama hali ya hewa m yajua kali.
  • Kupunguza MicheMimea ya karoti inahitaji kupunguzwa mara mbili. Mara ya kwanza hupunguzwa ikiwa na majani matatu mpaka manne au wiki mbili tangu kupandwa na kuachwa katika nafasi ya sentimita tano mpaka saba. Mara ya pili hupunguzwa ikiwa na urefu wa sentimita 10 mpaka 13, na kuachwa katika nafasi ya sentimita 10 mpaka 15. Karoti zilizopunguzwa zinaweza kutumika kwa chakula.
  • PaliziZao la karoti linahitaji kupaliliwa mara kwa mara. Palilia kwa kupandishia udongo na kuwa mwangalifu ili usikate mizizi.
  • MboleaWeka mbolea ya chumvichumvi aina ya S/A kama mbolea za asili hazikutumika wakati wa kupanda. Kiasi kinachotakiwa ni kilo 100 kwa hekta. Weka kilo 50 kwa hekta iwapo mbolea za asili zimetumika. Mbolea iwekwe wakati wa kupunguza miche mara ya pili. Weka katikati ya mistari na kwenye mifereji na kisha fukia.
Kuzuia Magonjwa na Wadudu Waharibifu:
Magonjwa:
  • Madoajani (Leaf Spot)Ugonjwa huu husababishwa na ukungu na hutokea wakati karoti zina urefu wa sentimita 13 mpaka 15. Hushambulia majani na kuyafanya yawe na madoa yenye rangi nyeusi iliyochanganyika na kijivu au kahawia. Sehemu zinazozunguka madoa haya hubadilika rangi na kuwa njano. Ugonjwa ukizidi majani hukauka. Zuia ugonjwa huu kwa kunyunyizia dawa za ukungu kama vile Dithane-M 45, Blitox, Copperhydroxide (Kocide), Copper Oxychloride, Cupric Hydroxide (Champion), Antrocol, Topsin M- 70% na Ridomil.
  • Kuoza Mizizi (Sclerotinia Rot).
    Ugonjwa huu husababishwa na ukungu na hushambulia mizizi namajani. Dalili zake ni kuoza kwa mizizi na majani. Baadaye sehemu hizi hufunikwa na uyoga mweupe. Kwenye uyoga huu huota siklerotia kubwa zenye rangi nyeusi.Zuia ugonjwa huu kwa kuzingatia yafuatayo:-
    - Epuka kustawisha karoti kwenye maeneo yaliyoshambuliwa na ugonjwa huu.
    - Nyunyuzia dawa za ukungu kama vile Dithane M- 45, Blitox, Topsin - M 70% na Ridomil.
  • Madoa Meusi (Black Leaf Spot)Huu pia ni ugonjwa wa ukungu unaoshambulia majani na mizizi. Majani yaliyoshambuliwa huwa na rangi ya manjano ambayo baadaye hubadilika na kuwa kahawia. Mizizi huwa na madoa meusi yaliyodidimia. Ugonjwa huu unaweza kuzuiwa kwa kutumia mbegu zilizothibitishwa kitaalamu, kubadilisha mazao na kuepuka kujeruhi karoti wakati wa kupalilia, kuvuna au kusafirisha.
Wadudu
  • Minyoo FundoMinyoo hii hushambulia mizizi na kuifanya iwe na vinundu. Hali hii husababisha mmea kudumaa na kupunguza mavuno. Minyoo fundo huweza kuzuiwa kwa kubalidilisha mazao. Baada ya kuvuna usipande mazao yajamii ya karoti au mazao yanayoshambuliwa na wadudu hawa. Unawezakupandamazao ambayo bayashambuliwi na minyoo fundo kama vile mahindi. Pia hakikisha shamba ni safi wakati wote.
  • Imi wa KarotiMashambulizi hufanywa na funza ambaye hutoboa mizizi. Ili kuzuia wadudu hawa tumia dawa kama vile Dichlorvos, Sapa Diazinon na Fenvalerate. Pia badilisha mazao na wakati wa kupalilia pandishia udongo kufunika mizizi.
  • Karoti Kuwa na Mizizi Mingi (Folking)
    Hii hutokea kama karoti zimepandwa kwenye udongo wenye takataka nyingi na usiolainishwa vizuri. Vile vile utumiaji wa mbolea za asili zisizooza vizuri unaweza kusababisba karoti kuwa na mizizi mingi. Hali hii inaweza kuzuiwa kwa kulainisha udongo vizuri na kutumia mbolea za asili zilizooza vizuri.
KUVUNA
Karoti huwa tayari kwa kuvunwa baada ya wiki 10 hadi 12 tangu kupandwa kutegemea hali ya hewa. Wastani wa mavuno kwa hekta moja ni tani 25 au zaidi.

Comments

Popular posts from this blog

Utengenezaji wa Chakula cha Kuku wa Nyama (Bloilers)

Utangulizi Kuku wa nyama wana mahitaji yafuatayo ya viinilishe katika chakula ili wakue vizuri Viinilisha vya wanga 60-65%   Protini 30-35%   Madini 2-8% Chakula cha Vifaranga Chakula hiki hutengenezwa katika namna ya kumsaidia kifaranga aweze kumeza vizuri na hivyo hakitakiwi kuwa katika punje punje. Hata kama utanunua pumba, ni vema kuzipitisha kwenye mashine ili ziwe laini zaidi.  Mahitaji (kgs)  Unga wa dona wa nafaka kama mahindi au mtama 40  Pumba za mtama au mahindi au uwele 27  Mashudu ya alizeti au ufuta, au pamba au karanga n.k. 20  Unga wa mifupa au chokaa ya kuku (DCP) 2.25  Dagaa au mabaki ya samaki (sangara fish meal) 10  Chumvi ya jikoni 0.5  Virutubisho (Broiler premix) 0.25  Jumla utapata 100Kg. Chakula cha kukuzia – growers mash Mahitaji (Kg) Mahindi yaliyobarazwa au mtama au uwele 25   Pumba za mtama au mahindi au uwele 44   Mashudu ya alizeti au ufuta, au pamba au karanga n.k. 17   Unga wa mifupa a...

Aina Za Miti ya Minazi

AINA ZA MINAZI Inafaa mkulima kufahamu kuna aina mbali mbali za minazi na ina mahitaji tofauti katika ukuaji. Ujuzi huu utamsaidia katika kuchagua aina ya minazi itakayofaa kwa eneo lake na kwa kiwango chake cha utunzaji. KUNA AINA TATU ZA MINAZI Minazi mirefu ya asili Minazi mifupi Minazi chotara MINAZI MIREFU YA ASILI (EAT) Minazi ya aina hii ndiyo inayojulikana na wakulima wengi kwa vile ni ya kiasili na imezoea mazingira yetu. Minazi hii huchukua miaka 6-8 tangu kupandikizwa hadi kuzaa. Minazi ya aina hii huvumilia ukame na inao uwezo wa kutoa wastani wa nazi 40 kwa mwaka. Nazi huwa kubwa na zenye nyama nene ambayo inafaa kwa kupikia na kukamua mafuta. Minazi hii huishi kad ya miaka 60 na kuendelea. Nchini Tanzania, minazi hii hustawi vyema ukanda wa pwani sehemu zisizo na mawe na ambazo hazituamishi maji. MINAZI MIFUPI (DWARF) Minazi ya aina hii huzaa mapema kuanzia miaka miwili. Huzaa nazi nyingi na ndogo. Nazi hizi huwa na nyama nyembamba hivyo hutumika kwa nnadafu. Minazi huhit...

Kilimo Bora cha Migomba

UTANGULIZI Hapa Tanzania kilimo cha migomba kimekuwepo Kwa miaka mingi. Kilimo hiki ni maarufu sana kwa sababu zao la ndizi limekuwa likitumika kama chakula kikuu kwa baadhi ya mikoa kama vile Kagera, Kilimanjaro na Mbeya na hivyo kulifanya muhimu, kufuatia mazao ya mahindi, mpunga, mtama, muhogo,viazi na mazao ya jamii ya kunde kama vile maharage. Zao la ndizi linaweza kuwa moja kati ya mazao ya biashara iwapo litazalishwa kwa kufuata kanuni bora za uzalishaji wa zao hilo, ikwa ni pamoja na kupanda aina bora ya migomba inayozaa ndizi zinazotambulika katika masoko ya kimataifa. ASILI YA MIGOMBA Asili ya migomba ni nchi za Malaysia na India ambazo ziko Kusini Mashariki mwa Asia. Migomba inayolimwa sasa imetokana na migomba ijulikanayo kama Musa balbisiana ambayo asili yake ni India, na Musa acuminata ambayo asili yake ni Malaysia. Kutoka Malaysia na India migomba ilifika Afrika Mashariki katika karne ya tano MAENEO YANAYOLIMWA MIGOMBA NCHINI Nchini Tanzania mikoa inayoshughulika na kili...