Skip to main content

Kilimo cha Mboga Mboga - Kabichi


UTANGULIZI
Nchini Tanzania kabichi hustawishwa zaidi katika mikoa ya Kilimanjaro, Arusha, Morogoro, Tanga, Iringa na Mbeya. Kabichi ina madini aina ya chokaa, kambakamba, protini na maji kwa wingi. Mboga hii inaweza kuliwa bila kupikwa au kuchemshwa kwa kutengeneza kachumbari. Pia inaweza kupikwa pamoja na vyakula kama vile nyama na maharagwe.

MAZINGIRA
Kabichi ni zao linalopendelea hali ya ubaridi. Zao hili hustawi na kutoa mazao mengi na bora kwenye sehemu zenye miinuko ya kuanzia mita 1200 hadi 1900 kutoka usawa wa bahari.
Hustawi vizuri kwenye udongo wa kitifutifu wenye rutuba nyingi na uwezo wa kuhifadhi unyevu kwa muda mrefu. Vilevile linaweza kustawi katika aina nyingi za udongo ili mradi udongo huo usituamishe maj i na usiwe na chumvi nyingi. Endapo udongo hauna rutuba ya kutosha uongezewe mbolea za asili kama vile mbolea ya kuku, samadi na mbolea vunde.

AINA
Zifuatazo ni aina za kabichi zinazolimwa hapa nchini:-
  • Prize Drumhead
    Vichwa vyake ni vikubwa (Kilo 2.0 mpaka 2.5) na bapa. Huchelewa kukomaa (Siku 110 hadi 120) tangu kupandikiza miche na hupasuka kirahisi. Aina hii huvumilia hali ya jua kali.
  • Early Jersey Wakefleld
    Aina hii inazaa kabichi zenye umbo lililochongoka kidogo (koniko) na zinazofunga vizuri. Kabichi moja inaweza kufikia uzito kati ya kilo 1.5 hadi 2.0. Hukomaa mapema (siku 90 hadi 100) tangu kupandikiza miche.
  • Copenhagen Market
    Vichwa vya Copenhagen Market ni vya mviringo na hupasuka kirahisi. Aina hii pia hukomaa mapema (siku 90 hadi 100) tangu kupandikiza miche.
  • Oxheart
    Kabichi zake ni ndogo zilizochongoka mfano wa moyo wa ng'ombe. Zinapendwa sana na walaji kutokana na ladha yake tamu. Hukomaa mapema na hazipasuki.
  • Glory of Enkhuizen
    Vichwa vyake ni vya mviringo. Aina hii huvumilia hali ya juakali, lakinihuchelewakukomaa (siku 110 hadi 120) tangu kupandikiza miche na haivumilii hali ya kupasuka.
  • Aina nyingine ni Brunswick na Danish Ball head.
KUBADILISHA MAZAO
Kabichi ni zao linalotumia virutubisho vingi ardhini kulinganisha na mboga zingine. Hivyo kabla ya kustawishwa, panda mazao jamii ya mikunde ili kuongeza rutuba. Halikadhalika baada ya kuvuna panda mazao yanayotumia chakula kidogo kama vile Karoti, Radishi au Lettuce. Kubadilisha mazao pia hupunguza kuenea kwa wadudu waharibifu na magonjwa.

KUOTESHA MBEGU
Mbegu huoteshwa kwanza kitaluni na baadae miche huhamishwa shambani. Lima vizuri sehemu itakayooteshwa mbegu. Weka mbolea za asili zilizooza vizuri kiasi cha ndoo tano mpaka 10 zenye ujazo wa lita 20 kwa eneo la mita mraba 10. Changanya vizuri mbolea na udongo, kisha lainisha udongo kwa kuvunjavunja mabonge makubwa, kwa kutumia reki au kifaa chochote. Baada ya kulainisha udongo, tengeneza tuta lililoinuliwa kiasi na lenye upana wa mita moja. Mwagilia tuta siku moja kabla ya kusia mbegu ili kuloanisha udongo. Tengeneza mistari katika tuta hilo yenye nafasi ya senumita 10 mpaka 15 kutoka mstari hadi mstari. Sia mbegu katika mistari hiyo na katika kina cha nusu sentimita mpaka 1.0. Kiasi cha mbegu kinachohitajika ni gramu moja katika eneo la mita mraba moja. Gramu 200 mpaka 300 za mbegu zinatosha kupandikiza katika eneo la hekta moja.
Funika mbegu kwa udongo au mbolea laini, kisha tandaza nyasi kavu ili kuhifadhi unyevu. Mwagilia maji kila siku asubuhi na jioni mpaka mbegu zitakapoota. Mbegu huota baada ya siku tano hadi 10. Umwagiliaji utategemea hali ya hewa. Kama kuna mvua hakuna haja ya kumwagilia kila siku.

KUTAYARISHA SHAMBA
Shamba litayarishwe mwezi mmoja kabla ya kupandikiza miche kwa kukatua ardhi hadi kufikia kina cha sentimita 30. Lainisha udongo na tengeneza matuta. Weka mbolea za asili zilizooza vizuri kiasi cha ndoo moja hadi mbili, kwa eneo la mita mraba 10. Mbolea hii iwekwe katika kila shimo. Kiasi kinachotakiwa ni kilo moja au kopo moja la Tanbond kwa kila shimo. Hii ni sawa kuweka na tani 10 hadi 20 kwa hekta. Katika sehemu zenye upungufu wa madini ya fosiforasi mbolea aina ya N.P.K yenye uwiano wa 5:15:5 itumike. Kiasi kinachotakiwa ni kijiko kimoja cha chai chenye gramu 5 kwa kila shimo la mche.

KUPANDIKIZA MICHE
Miche huwa tayari kwa kupandikizwa shambani baada ya majuma 3 hadi 5 tangu kuotesha mbegu, kutegemea aina ya kabichi. Wakati huu miche huwa na urefu wa sentimita 15 mpaka 20 au urefu ulio sawa na kalamu ya risasi. Ng'oa miche kwa uangalifu na pandikiza kama ilivyokuwa kitaluni Wakati wa kuweka miche shimoni hakikisha mizizi haipindi. Nafasi ya kupandikiza inategemea aina ya kabichi. Kabichi zenye vichwa vikubwa kama vile Drumhead zipandikizwe katika nafasi ya sentimita 60 kati yamche na mche na sentimita 75 kati ya mstari na mstari. Aina yenye vichwa vidogo kama vile Oxheart zipandikizwe katika nafasi ya sentimita 40 hadi 50 kutoka mche hadi mche na sentimita 60 kutoka mstari hadi mstari. Nafasi kati ya tuta na tuta lingine ni sentinuta 60. Wakati mzuri wa kupandikiza ni asubuhi aujioni. Baada ya kupandikiza weka matandazo kama vile nyasi kavu ili kuzuia magugu yasiote na kuhifadhi unyevu wa udongo.
Kupandikiza miche safu mbili katika tuta moja

Kupandikiza mche mmoja katika tuta noja

KUTUNZA BUSTANI

Palizi
Kabichi ni zao ambalo mizizi yake haina kina kirefu, hivyo palizi haina budi kufanyika juu juu ili kuepuka kuikata mizizi. Punguza palizi ya mara kwa mara kwa kuongeza matandazo hasa kabichi zinapoaza kufunga.

Umwagiliaji:
Kabichi hustawi vizuri zaidi iwapo kuna maji ya kutosha kwenye udongo. Mwagilia mara mbili au zaidi kwa wiki kutegemea hali ya hewa na aina ya udongo. Kabichi ambazo hazikupata maji ya kutosha huchelewa kufunga na huwa na vichwa vidogo. Zikikosa maji kwa muda mrefu na zikapata maji mengi ghafla, vichwa hupasuka.

Mbolea
Mbolea ya kukuzia (S/A) huwekwa shambani katika wiki ya nne hadi ya sita baada ya kupandikiza miche na kabla ya vichwakufunga. Weka kiasi cha kilo 200 kwa hekta. Mbolea hii iwekwe mara mbili; kilo 100 ziwekwe katika wiki ya nne hadi ya sita baada ya kupandikiza miche, kutegemea aina ya kabichi. Kiasi kinachobakia kiwekwe mwezi mmoja baadae. Kiasi kinachohitajika kwa mche ni kijiko kidogo chenye gramu tano. Mbolea iwekwe kuzunguka shina umbali wa sentimita 10 mpaka 15 kutoka kwenye shina, kwa aina ya vichwa vikubwa. Aina ya vichwa vidogo umbali uwe sentimita tano mpaka 10

ZINGATIA
Epuka kuweka mbolea nyingi, kwani husababisha vichwa visifunge vizuri (kabichi zinakuwa nyepesi).

Wadudu Waharibifu na Magonjwa

Wadudu:-
  • Viwavi wa Kabichi (Diamond Backmoth)
    Viwavi hawa huwa na rangi ya kijani kibichi na alama ya mstari wa kung'aa mgongoni, Nondo hutaga mayai chini yajani na baada ya kuanguliwa viwavi hula sehemu ya chini yajani na kuacha ngozi nyembamba mfano wa dirisha la kioo. Ni muhimu kuuwa viwavi kwa sababu ndiyo wanaoleta madhara makubwa.
    Wadudu hawa wanaweza kuzuiwa kwa kunyunyuzia moja ya dawa zifuatazo:- Nogos, Pennethrin, Dimethoate, Sevin W.P. na Sumicidin.
  • Inzi wa Kabichi (Cabbage Sawfly)
    Mashambulizi hufanywa na kiluwiluwi mwenye rangi ya kijani kibichi au bluu. Hula majani yote ya kabichi na kubakisha vena au vishipa vya majani.
    Inzi wa kabichi wanaweza kuzuiwa kwa kutumia dawa za Caibaryl (Sevin), Dimethoate (Dimethoate Sapa), Pennethrin, na Fenvalerate (Sumicidin).
  • Sota (Cutworms)
    Hawa ni funza wakubwa wenye rangi ya kijivu. Hupendelea kujichimbia katika udongo wakati wa mchana na kukata miche michanga karibu na usawa wa ardhi wakati wa usiku.
    Zuia wadudu hawa kwa kutumia majivu au dawa kama vile Carbaryl, Fenvalerate, na Deltamethrin (Decis) mara baada ya kupanda. Kama mche utakatwa, mtoe mdudu huyu kwa kumfukua na kumuua. Kisha pandikiza mche mwingine.
  • Vidukari au Wadudu Mafuta (Cabbage Aphids)
    Wadudu hawa ni wadogo sana wenye rangi ya kijani, nyeusi au khaki. Baadhi yao wana mabawa na wengine hawana. Hufyonza utomvu wa mimea na husababisha majani kubadilika rangi na kuwa meupe au njano iliyopauka. Mmea hudumaa na hatimaye hukauka.Wazuie wadudu hawa kwa kunyunyizia mojawapo ya dawa zifuatazo:- Fenvalerate, Dimethoate, Lambda - Cyhalothrin (Karate) na Dichlorvos (Nogos).
  • Minyoo Fundo (Root knot Nematodes)
    Hawa ni wadudu wadogo wanaoishi ardhini na ambao hawaonekani kirahisi kwa macho. Hushambulia mizizi na kusababisha kabichi kudhoofu na hushindwa kufunga vizuri. Mimea iliyoshambuliwa mizizi yake huwa na nundunundu.
    Wadudu hawa wanaweza kuzuiwa kwa kuzingatia yafuatayo:-
    - Utumiaji wa mbolea za asili kila msimu hupunguza kuzaliana kwa wadudu hawa.
    - Usipande kabichi mfululizo kwenye sehemu ile ile wala jamii yake kama vile kabichi ya kichina na kolifulawa, ila badilisha kwa kupanda mazao mengine kama vile mahindi, karoti, radishi na vitunguu.
    - Ondoa masalia yote shambani ambayo yanaweza kueneza wadudu hawa na yachome moto.
  • African Mole Cricket
    Hawa ni aina ya panzi ambao hujificha kwenye nyufa za udongo mchana. Hujitokezajuu usiku kwa kuchimba udongo kutumia miguuyambele. Wadudu, hawa huharibu mizizi na hula majani ya miche michanga.
    Zuia wadudu hawa kwa kutumia dawa ya Carbaryl. Changanya gramu 50 (vijiko vitano vikubwa vya chakula) vya dawa pamoja na kilo moja ya mchele, mtama au pumba za mahindi au ngano. Ongeza maji kidogo kwenye mchanganyiko huo na kisha mwaga kwenye njia wanazopita wadudu hawa.
Magonjwa
  • Kwza Shingo (Bacterial Softrot)
    Ugonjwa huu husababishwa na vijidudu vya bakteria ambavyo viko kwenye udongo. Hushambulia kabichi na kuzifanya zibadilike rangi, kuoza na kutoa harufu mbaya. Vijidudu vidogo vidogo pia huonekana kwenye sehemu iliyooza.
    Zuia ugonjwa huu kwa kuzingatia yafuatayo:-
    - Epuka kujeruhi kabichi wakati wa kuvuna
    - Vuna kabichi wakati hakuna mvua.
    - Usilundike kabichi kwa wingi na kwa muda mrefu.
    - Hifadhi kwenye sehemu yenye ubaridi na yenye kuingiza hewa ya kutosha
    - Ng'oa masalia, choma moto na lima shamba mara moja baada ya kuvuna.
    - Badilisha mazao.
  • Uozo Mweusi (Blackrot)
    Huu pia ni ugonjwa unaosababishwa na vijidudu vya backteria na hushambulia sana kabichi. Dalili kubwa za ugonjwa huu ni majani kugeuka rangi na kuwa ya njano na baadae kikahawia. Majani huanza kunyauka toka kwenye kingo zake na kuacha alama ya "V". Kingo zinakuwa na rangi nyeusi isiyokolea. Baadaye majani yaliyoshambuliwa hudhoofika na kupukutika. Kama ukikata jani au shina, mviringo mweusi huonekana kwenye vena. Ugonjwa huu unaweza kuzuiwa kwa kuzingatia yafuatayo:-
- Badilisha mazao kwa muda wa miaka miwili usipande kabichi najamii yake.
- Panda kabichi kwenye sehemu ambayo haituamishi maji.
- Kitalu na mazingira yawe safl daima.
- Punguza miche ili kupunguza msongamano.
- Ondoa masalia yote ya kabichi shambani baada ya kuvuna na yachome moto.
- Panda mbegu zilizothibitishwa na wataalamu.
  • Kuoza Shina (Black leg)
    Ugonjwa huu chanzo chake ni ukungu. Dalili kubwa za ugonjwa huu ni kuwepo kwa madoa yaliyodidimia yenye rangi ya kikahawia kwenye shina karibu na usawa wa ardhi, ikifuatiwa na kuvimba kwa shina. Baadaye uyoga mweusi huonekana kwenye uvimbe huo. Pia uozo wa rangi ya kikahawia huonekana ndani ya shina. Kwenye majani huonekana madoa meusi ya mviringo yaliyozungukwa na uyoga mweusi. Zuia ugonjwa huu kwa kuzingatia yafuatayo:-
- Panda katika sehemu ambayo haituamishi maji.
- Badilisha mazao; kwa muda wa miaka mitatu usipande zao la kabichi na jamii yake
- Lima shamba mara baada ya kuvuna ili kuwezesha masalia ya mazao kuoza haraka kabla ya kupanda.
- OndOa kabichi zote zilizoshambuliwa shambani.
- Tumia dawa za kuzuia magonjwa ya ukungu kama vile Ridomil.
  • Uvimbe wa Mizizi (Clubroot)
    Huu pia ni ugonjwa unaosababishwa na kuvu au ukungu. Hushambulia mizizi na dalili zake ni kudumaa kwa mmea na majam kukunjamana. Baadae mmea huoza.
    Ugonjwa huu unaweza kuzuiwa kwa kubadilisha mazao.
  • Madoajani Meusi (Black Leaf Spot)
    Chanzo cha ugonjwa huu ni ukungu. Dalili zake m kuonekana kwa madoa madogo ya mviringo yenye rangi ya njano kwenye majani. Baadae madoa haya huwa makubwa na hugeuka kuwa meusi.
    Zuia ugonjwa huu kwa kuzingatia yafuatayo:-
- Badilisha mazao
- Hakikisha shamba ni safi wakati wote.
- Ikibidi tumia dawa za ukungu kama vile Copperhydroxide (Kocide),Copper Oxychloride (Cupro).
  • Ubwiri Vinyoya (Downy Mildew)
    Huu ni ugonjwa wa ukungu ambao hupendelea sana hali ya unyevunyevu na baridi kali na huonekana zaidi kwenye kitalu. Dalili zake ni majani kuwa na mabaka ya mviringo yenye njano upande wa juu. Baadaye mabaka haya hubadilika na kuwa na rangi ya zambarau iliyochanganyika na nyeupe upande wa chini wa majani.
    Ugonjwa huu unaweza kuzuiwa kwa kutumia njia zifuatazo:-
- Kilimo cha kubadilisha mazao
- Hakikisha udongo hautuamishi maji na kitalu ni kisafi wakati wote.
- Nyunyizia dawa za ukungu kama vile Zineb, Dithane M - 45, Copperhydroxide (Kocide) na Copper Oxychloride, Topsin -M na Ridomil.
  • Kuoza Shina au Kinyawhi (Dampmg offor End Wire Stem)
    Husababishwa na ukungu na hushambulia miche michanga. Miche iliyoshambuliwa huonyesha dalili za kunyauka, baadae huanguka na kukauka. Miche mikubwa huonyesha dalili za kudumaa. Sehemu ya shina iliyokaribu na ardhi hulainika na kuwa na rangi ya kikahawia.
    Ugonjwa huu unaweza kuzuiwa kwa kutumia njia zifuatazo
- Punguza miche kama imesongamana.
- Nyunyizia dawa za ukungu kama vile Dithane M - 45, Ridomil, Thiophanate (Topsin - M).
KUVUNA NA KUHIFADHI
Kuvuna
Kabichi hukomaa na huvunwa baada ya siku 60 mpaka 120 kutegemea aina iliyostawishwa tangu kupandikiza miche. Uvunaji hufanyika kwa kukata shina sentimita mbili hadi tatu kutoka kwenye kichwa kwa kutumia kisu. Ondoa majani ya nje na acha majani mawili au matatu ya kijani kwa ajili ya kuzuia kabichi zisikwaruzike na kuoza wakati wa kusafirisha. Punguza nusu ya urefu wa majani ya nje ili kurahisisha ufungaji. Kwa kawaida uvunaji hufanyika wakati wa asubuhi aujioni. Kiasi cha tani 40 au zaidi za kabichi kwa hekta hupatikana kama zao limetunza vizuri. Ondoa kabichi zilizooza au kuharibika wakati wa kuvuna. Kisha panga zilizobaki kufuata daraja kama vile ndogo, za kati na kubwa.

Hifadhi
Kabichi ni zao linaloharibika kwa haraka, hivyo halina budi kutumika mapema iwezekanavyo baada ya kuvuna. Kabichi kwa ajili ya kuuzwa zisafirishwe mara moja kwa walaji. Kama usafiri ni mgumu, zihifadhiwe kwenye sehemu yenye ubaridi na hewa ya kutosha. Wakati wa kusafirisha, ziwekwe kwenye matenga au visanduku vya mbao vilivyo na matundu yanayoingiza hewa ya kutosha.

Comments

Post a Comment

Popular posts from this blog

Utengenezaji wa Chakula cha Kuku wa Nyama (Bloilers)

Utangulizi Kuku wa nyama wana mahitaji yafuatayo ya viinilishe katika chakula ili wakue vizuri Viinilisha vya wanga 60-65%   Protini 30-35%   Madini 2-8% Chakula cha Vifaranga Chakula hiki hutengenezwa katika namna ya kumsaidia kifaranga aweze kumeza vizuri na hivyo hakitakiwi kuwa katika punje punje. Hata kama utanunua pumba, ni vema kuzipitisha kwenye mashine ili ziwe laini zaidi.  Mahitaji (kgs)  Unga wa dona wa nafaka kama mahindi au mtama 40  Pumba za mtama au mahindi au uwele 27  Mashudu ya alizeti au ufuta, au pamba au karanga n.k. 20  Unga wa mifupa au chokaa ya kuku (DCP) 2.25  Dagaa au mabaki ya samaki (sangara fish meal) 10  Chumvi ya jikoni 0.5  Virutubisho (Broiler premix) 0.25  Jumla utapata 100Kg. Chakula cha kukuzia – growers mash Mahitaji (Kg) Mahindi yaliyobarazwa au mtama au uwele 25   Pumba za mtama au mahindi au uwele 44   Mashudu ya alizeti au ufuta, au pamba au karanga n.k. 17   Unga wa mifupa a...

Aina Za Miti ya Minazi

AINA ZA MINAZI Inafaa mkulima kufahamu kuna aina mbali mbali za minazi na ina mahitaji tofauti katika ukuaji. Ujuzi huu utamsaidia katika kuchagua aina ya minazi itakayofaa kwa eneo lake na kwa kiwango chake cha utunzaji. KUNA AINA TATU ZA MINAZI Minazi mirefu ya asili Minazi mifupi Minazi chotara MINAZI MIREFU YA ASILI (EAT) Minazi ya aina hii ndiyo inayojulikana na wakulima wengi kwa vile ni ya kiasili na imezoea mazingira yetu. Minazi hii huchukua miaka 6-8 tangu kupandikizwa hadi kuzaa. Minazi ya aina hii huvumilia ukame na inao uwezo wa kutoa wastani wa nazi 40 kwa mwaka. Nazi huwa kubwa na zenye nyama nene ambayo inafaa kwa kupikia na kukamua mafuta. Minazi hii huishi kad ya miaka 60 na kuendelea. Nchini Tanzania, minazi hii hustawi vyema ukanda wa pwani sehemu zisizo na mawe na ambazo hazituamishi maji. MINAZI MIFUPI (DWARF) Minazi ya aina hii huzaa mapema kuanzia miaka miwili. Huzaa nazi nyingi na ndogo. Nazi hizi huwa na nyama nyembamba hivyo hutumika kwa nnadafu. Minazi huhit...

Kilimo Bora cha Migomba

UTANGULIZI Hapa Tanzania kilimo cha migomba kimekuwepo Kwa miaka mingi. Kilimo hiki ni maarufu sana kwa sababu zao la ndizi limekuwa likitumika kama chakula kikuu kwa baadhi ya mikoa kama vile Kagera, Kilimanjaro na Mbeya na hivyo kulifanya muhimu, kufuatia mazao ya mahindi, mpunga, mtama, muhogo,viazi na mazao ya jamii ya kunde kama vile maharage. Zao la ndizi linaweza kuwa moja kati ya mazao ya biashara iwapo litazalishwa kwa kufuata kanuni bora za uzalishaji wa zao hilo, ikwa ni pamoja na kupanda aina bora ya migomba inayozaa ndizi zinazotambulika katika masoko ya kimataifa. ASILI YA MIGOMBA Asili ya migomba ni nchi za Malaysia na India ambazo ziko Kusini Mashariki mwa Asia. Migomba inayolimwa sasa imetokana na migomba ijulikanayo kama Musa balbisiana ambayo asili yake ni India, na Musa acuminata ambayo asili yake ni Malaysia. Kutoka Malaysia na India migomba ilifika Afrika Mashariki katika karne ya tano MAENEO YANAYOLIMWA MIGOMBA NCHINI Nchini Tanzania mikoa inayoshughulika na kili...