Skip to main content

Ufugaji na Utunzaji Wa Ndege Aina Ya Kwale



KWALE ni jamii ya ndege ambao kwa sasa wanafugwa majumbani na wanaotaga mayai kama kuku ama bata na kwa wingi sana. Ndege hawa ni wadogo 280gm - 300gm, Wanarangi ya brown, nyeusi au hata nyeupe yenye miraba na madoa ya rangi ya ugondo au kijivu. Manyoya yao pia yana rangi ya brown au nyeupe na yenye madoa yanayovutia.

Ufugaji wa KWALE ni njia bora na rahisi sana kwa mfugaji yeyote aliyetayari kukuza kipato chake kwa haraka sana na kwa kiwango cha juu.

Kutaga na kuatamia
KWALE dume humpanda jike kwa muda kidogo, Hapo jike anakuwa tayari kutaga na hutaga mayai 290 hadi 310 kwa mwaka (hii hulingana na lishe nzuri atakayopatiwa).
Mayai ya KWALE huatamiwa kwa siku 18 na huanza kuanguliwa vifaranga kwa muda wa siku 2, kuanzia siku ya 18 na hadi 20.

Njia bora ya kutotolesha mayai ya KWALE ni kwa kutumia incubator ambapo mayai huatamiwa kwa wingi ndani ya siku 18.
Utunzaji wa vifaranga na chakula:
Siku 1 – 7 
Vifaranga wapatiwe chakula “STARTER PELLET” na maji masafi ya kutosha. Siku ya 1 wawekee ‘GLUCOSE’ kwenye maji, Packet moja kwa lita 20 za maji, na siku ya pili hadi ya tano wawekee Amin Total kwenye maji, Wape maji pekee siku ya sita na siku ya saba wapatie chanjo ya Newcastle. Utawapatia joto kwa njia ya umeme kwa ‘BULB’ mbili (2) za 200watts kwa kila vifaranga 300, ama unaweza kuweka taa ya ‘Energy Server’ pamoja na jiko la mkaa uliofunikwa na majivu ambao utakidhi kuwapatia joto sawia kwa masaa 24 kwa siku 7. (Majivu yanasaidia moto kukaa kwa muda mrefu)
Banda/box lako liwe la ukubwa wa 1.5m x 1.5m (au eneo la ukubwa huo ndani mwa banda kubwa la kufugia kuku) lazima uzingatie usalama wa vifaranga dhidi ya panya, paka au vicheche. Unatakiwa kuweka ‘magazeti au mabox’ chini kwenye sakafu yatakayosaidia usafi. Kwa week ya kwanza chakula kitawekwa chini na tunashauri utumie chakula cha pellet ili kusaidia vifaranga wasiteleze na kuathiri miguu.
Siku 8-14
Vifaranga wataendelea kupewa chakula “STARTER PELLET” na maji safi. Wataendelea kuhitaji ‘mwanga’ wa kutosha muda wote na joto la wastani bulb 2 za watts 100 au moja ya watts 200
Siku 15-21
Uhitaji wa joto utapungua, ila ni kipindi ambacho wanakula chakula zaidi kwa ajili ya kukua. Ni vizuri waendelee kupata taa ili kupata mwangaza utakayowawezesha kula mchana na usiku.

Siku 21 na Kuendelea 
KWALE wako hawatahitaji joto tena wawekee taa tu za energy server kipindi cha usiku, wape chakula na maji ya kutosha zaidi kwa ajili ya kukua.
Utagaji Mayai, Wiki ya Sita
Wiki ya sita kuelekea ya saba KWALE wako wataanza kutaga mayai kila siku, kwa wastani KWALE mmoja hutaga mayai 300 kwa mwaka.
Magonjwa
KWALE ni ndege wenye kinga kubwa na ni vigumu sana kushambuliwa na magonjwa kama kuku na mara wanapougua ni rahisi sana kutibika. Magonjwa yanayoweza kuwapata KWALE ni typhoid, mafua na kuharisha .
Tiba za Asili
Waweza kuwatibu vifaranga au KWALE wako kwa kutumia njia ya asili ambayo pia ni rahisi, gharama nafuu na bora zaidi kuliko kutumia madawa yaliyochanganywa na kemikali na yenye gharama.
Vifuatazo ni vitu vya asili vinavyotumika kutibu magonjwa mbali mbali kwa KWALE na yanayopatikana kwa wingi katika maeneo ya mfugaji. Madawa haya hutumika kwa kiwango cha wastani na hayana kipimo maalum kwani hata ukiyazidisha hayana madhara.
Mwarobaini na Aloe Vera: Madawa haya hutumika kutibu kuharisha damu pamoja na mafua kwa vifaranga vya KWALE. Chukua kiasi kidogo cha mwarubaini kisha twanga vizuri kupata maji maji. Kamua maji yale, kisha weka katika maji uliyoandaa kuwanywesha vifaranga wako. Kata vipande vidogovidogo vya aloe vera (jani moja laweza kutosha) na tia katika maji yaliyochanganywa na mwarobaini, kisha wapatie vifaranga wanywe (Aloe Vera itaendelea kujikamua yenyewe ikiwa ndani ya maji huku vifaranga wakiendele kunywa).
Kitunguu Swaumu: Hii hutumika kukinga na kutibu vifaranga vya KWALE wanaosumbuliwa na kuharisha damu. Unachukua kitunguu swaumu na kuondoa maganda ya nje kisha kusafisha na kukata vipande vidogo sana, na kuwawekea kama chakula. Vifaranga wanapenda sana vitunguu hivyo na watakula kwa kasi kama chakula lakini ni tiba tayari. Unaweza kuwapatia kila siku hadi watakapo pona.
Maziwa:Maziwa yanayotokana na ng’ombe pia hutumika kutibu ugonjwa wa kuhara pamoja na kuwapa nguvu KWALE waliolegea. Mnyweshwe maziwa hayo KWALE anayeumwa bila kuyachemsha na umnyweshe maziwa ya kutosha kiasi cha kushiba. Unamnywesha mara tatu kwa siku. Hakikisha maziwa unayotumia yanatoka kwa ng’ombe wanaotibiwa kila mara.
Angalizo:
Siyo lazima KWALE waugue ndipo uwapatie tiba hizi. Hakikisha unawapa tiba kabla hata hawajaugua hivyo utawakinga na magonjwa hayo. Waweza kuchanganya madawa hayo yote kwa wakati mmoja kwani hayana madhara.
Endapo madawa ya asili hayapatikani katika eneo la mfugaji basi waweza kuwatibu KWALE kwa madawa yafuatayo ambapo vipimo huelezwa moja kwa moja kwa maandishi katika madawa hayo au kuelezwa na muuzaji pale utakaponunulia; Amprolium kwa ugonjwa wa kuharisha damu (Coccidiosis), Fluban,Coridix au Doxyco kutibu mafua (Coryza) na Esb3,Trisulmycine au Trimazine hutumika kwa homa ya matumbo (Typhoid).
Chanjo:
Siku ya 7
lazima vifaranga wapatiwe chanjo ya “kideri/mdondo” (respiratory & digestive diseases) kwa dawa inayoitwa ‘newcastle’. Chanzo cha maambukizi ni maji na chakula kilichochafuliwa na kinyesi na pia husababishwa na virusi kwa njia ya hewa.
Siku ya 14
lazima wapewe chanjo ya “gumboro”. Chanzo cha maambukizi ni maji na chakula kilichochafuliwa na kinyesi na pia husababishwa na virusi kwa njia ya hewa.
Siku ya 21 l
lazima warudie chanjo ya “Newcastle (aina ya IBDL)”. Chanzo cha maambukizi ni maji na chakula kilichochafuliwa na kinyesi na pia husababishwa na virusi kwa njia ya hewa.
Siku ya 35
lazima wapate chanjo ya “Ndui”.



Comments

Popular posts from this blog

Utengenezaji wa Chakula cha Kuku wa Nyama (Bloilers)

Utangulizi Kuku wa nyama wana mahitaji yafuatayo ya viinilishe katika chakula ili wakue vizuri Viinilisha vya wanga 60-65%   Protini 30-35%   Madini 2-8% Chakula cha Vifaranga Chakula hiki hutengenezwa katika namna ya kumsaidia kifaranga aweze kumeza vizuri na hivyo hakitakiwi kuwa katika punje punje. Hata kama utanunua pumba, ni vema kuzipitisha kwenye mashine ili ziwe laini zaidi.  Mahitaji (kgs)  Unga wa dona wa nafaka kama mahindi au mtama 40  Pumba za mtama au mahindi au uwele 27  Mashudu ya alizeti au ufuta, au pamba au karanga n.k. 20  Unga wa mifupa au chokaa ya kuku (DCP) 2.25  Dagaa au mabaki ya samaki (sangara fish meal) 10  Chumvi ya jikoni 0.5  Virutubisho (Broiler premix) 0.25  Jumla utapata 100Kg. Chakula cha kukuzia – growers mash Mahitaji (Kg) Mahindi yaliyobarazwa au mtama au uwele 25   Pumba za mtama au mahindi au uwele 44   Mashudu ya alizeti au ufuta, au pamba au karanga n.k. 17   Unga wa mifupa a...

Aina Za Miti ya Minazi

AINA ZA MINAZI Inafaa mkulima kufahamu kuna aina mbali mbali za minazi na ina mahitaji tofauti katika ukuaji. Ujuzi huu utamsaidia katika kuchagua aina ya minazi itakayofaa kwa eneo lake na kwa kiwango chake cha utunzaji. KUNA AINA TATU ZA MINAZI Minazi mirefu ya asili Minazi mifupi Minazi chotara MINAZI MIREFU YA ASILI (EAT) Minazi ya aina hii ndiyo inayojulikana na wakulima wengi kwa vile ni ya kiasili na imezoea mazingira yetu. Minazi hii huchukua miaka 6-8 tangu kupandikizwa hadi kuzaa. Minazi ya aina hii huvumilia ukame na inao uwezo wa kutoa wastani wa nazi 40 kwa mwaka. Nazi huwa kubwa na zenye nyama nene ambayo inafaa kwa kupikia na kukamua mafuta. Minazi hii huishi kad ya miaka 60 na kuendelea. Nchini Tanzania, minazi hii hustawi vyema ukanda wa pwani sehemu zisizo na mawe na ambazo hazituamishi maji. MINAZI MIFUPI (DWARF) Minazi ya aina hii huzaa mapema kuanzia miaka miwili. Huzaa nazi nyingi na ndogo. Nazi hizi huwa na nyama nyembamba hivyo hutumika kwa nnadafu. Minazi huhit...

Kilimo Bora cha Migomba

UTANGULIZI Hapa Tanzania kilimo cha migomba kimekuwepo Kwa miaka mingi. Kilimo hiki ni maarufu sana kwa sababu zao la ndizi limekuwa likitumika kama chakula kikuu kwa baadhi ya mikoa kama vile Kagera, Kilimanjaro na Mbeya na hivyo kulifanya muhimu, kufuatia mazao ya mahindi, mpunga, mtama, muhogo,viazi na mazao ya jamii ya kunde kama vile maharage. Zao la ndizi linaweza kuwa moja kati ya mazao ya biashara iwapo litazalishwa kwa kufuata kanuni bora za uzalishaji wa zao hilo, ikwa ni pamoja na kupanda aina bora ya migomba inayozaa ndizi zinazotambulika katika masoko ya kimataifa. ASILI YA MIGOMBA Asili ya migomba ni nchi za Malaysia na India ambazo ziko Kusini Mashariki mwa Asia. Migomba inayolimwa sasa imetokana na migomba ijulikanayo kama Musa balbisiana ambayo asili yake ni India, na Musa acuminata ambayo asili yake ni Malaysia. Kutoka Malaysia na India migomba ilifika Afrika Mashariki katika karne ya tano MAENEO YANAYOLIMWA MIGOMBA NCHINI Nchini Tanzania mikoa inayoshughulika na kili...