Utangulizi Mifugo ni rasilimali ambayo huwapa faida kubwa wafugaji na wananchi kwa ujumla. Ili mifugo itoe mazao yenye tija inahitaji kupatiwa huduma bora za malisho, maji, kinga na tiba za maradhi. Maradhi ni moja kati ya matatatizo yanayozorotesha sekta ya ufugaji na kupunguza uzalishaji. Katika kukabiliana na changamoto hiyo hatua za kuyadhibiti maradhi zinachukuliwa duniani kote ili kuimarisha ufugaji na kupata tija. Chanjo Chanjo ni mchanganyiko maalum wenye vijidudu ambavyo vimepunguzwa nguvu ili visilete madhara kwa wanyama au watu waliochanjwa. Hii ni njia mojawapo inayotumika katika kudhibiti maradhi duniani. Asili ya chanjo ilitokana na ugunduzi wa mwanasayansi wa Uingereza Bw. Edward Jenner katika karne ya 18 ambapo aligundua kwamba wahudumu wa ng’ombe hawakupata ugonjwa aina ya ndui (small pox) kutokana na kuwa na vijidudu vya ugonjwa wa ndui za ng’ombe (cow pox) hali ya kuwa maeneo mengine wasiokuwa wahudumu wa ng’ombe waligundulika kuwa na ugonjwa huo. Chan...