Mbuzi na kondoo wanaweza kufugwa kwa gharama nafuu na kuishi katika mazingira magumu kama ya maradhi na ukame ikilinganishwa na ng’ombe. Kutokana na umbile lao dogo wanaweza kufugwa katika eneo dogo na pia wanaweza kuhudumiwa na familia yenye nguvukazi na kipato kidogo. Uzao wa muda mfupi unamwezesha mfugaji kupata mbuzi/kondoo wengi kwa kipindi kifupi. Wanyama hao hufugwa kwa ajili ya nyama, maziwa, ngozi, sufu na mazao mengine kwa matumizi ya familia na kuongeza kipato.
Kanuni za kuzingatia
Ufugaji bora wa mbuzi na kondoo uzingatie kanuni zifuatazo:-
- Wafugwe kwenye banda au zizi bora,
- Wachaguliwe kutokana na sifa za koo/aina na lengo la uzalishaji (nyama, maziwa au sufu),
- Wapatiwe lishe sahihi kulingana na umri na mahitaji ya mwili,
- Kuzingatia mbinu za kudhibiti magonjwa kama inavyoshauriwa na mtaalam wa mifugo,
- Kuweka na kutunza kumbukumbu sahihi za uzalishaji; na
- Kuzalisha nyama, maziwa au sufu yenye ubora unaokidhi mahitaji ya soko
Mbuzi/kondoo wanaweza kufugwa katika mifumo ya huria, shadidi na kwa kutumia njia zote mbili. Zizi hutumika katika mfumo huria ambapo mbuzi/kondoo huchungwa wakati wa mchana na kurejeshwa zizini wakati wa usiku. Zizi bora ni lile lenye sifa zifuatazo:-
- Lililo imara linaloweza kumkinga mbuzi/kondoo dhidi ya wanyama hatari nawezi,
- Lililojengwa mahali pa mwinuko pasiporuhusu maji kutuama,
- Ukubwa wa zizi uzingatie idadi na umri wa mifugo. Ni vema mbuzi/kondoo watengwe kulingana na umri wao; na
- Liruhusu usafi kufanyika kwa urahisi.
- Imara, lenye uwezo wa kuwahifadhi kiafya na pia dhidi ya hali ya hewa hatarishi kwa mfano jua kali, upepo, baridi na mvua pamoja na wanyama hatari,
- Lenye mwanga, hewa na nafasi ya kutosha inayoruhusu usafi kufanyika kwa urahisi,
- Lijengwe sehemu isiyoruhusu maji kutuama na liwe mbali kidogo na nyumba ya kuishi watu. Pia ujenzi uzingatie mwelekeo wa upepo ili hewa kutoka bandani isiende kwenye makazi,
- Liwe na sakafu ya kichanja chenye urefu wa mita 1 kutoka ardhini (Kwa banda la mbuzi),
- Liwe na sehemu ya kuwekea chakula, maji na mahali pa kuweka jiwe la chumvichumvi; na
- Liwe na vyumba tofauti kwa ajili ya majike na vitoto, mbuzi/kondoo wanaokua, wanaonenepeshwa na wanaougua.
Inashauriwa banda la mbuzi/kondoo lijengwe kwa kutumia vifaa vinavyopatikana kwa urahisi katika eneo husika. Ukubwa wa banda utategemea idadi ya mbuzi/kondoo wanaofugwa humo na ukubwa wa umbo kama inavyoonekana
Eneo la mbuzi/kondoo linalotakiwa
Vitoto 0.3, Wasio na mimba 1.5, Wenye mimba 1.9, Dume 2.8, vipimo vyote ni kwa mita za mraba na ni kwa mbuzi mmoja
- Paa lijengwe kwa kutumia vifaa kama miti, mbao, na kuezekwa kwa nyasi, makuti, majani ya migomba, mabati au hata vigae kwa kutegemea uwezo wa mfugaji,
- Kuta zijengwe kwa kutumia mabanzi, mbao, nguzo, wavu wa waya, fito na matofali. Kuta ziwe imara zinazoruhusu hewa na mwanga wa kutosha. Mlango uwe na ukubwa wa sentimita 60 x 150
- Sakafu inaweza kuwa ya udongo au zege. Sakafu ya kichanja inaweza kujengwa kwa kutumia miti, fito, mianzi, mbao au mabanzi na iweze kuruhusu kinyesi na mkojo kupita. Chumba cha majike na vitoto kiwe na nafasi ya sentimita 1.25 kati ya papi na papi, fito na fito au mti hadi mti.
- Chumba cha mbuzi/kondoo wakubwa iwe sentimita 1.9 kati ya mbao na mbao.
Madhumuni ya kuchagua mbuzi au kondoo wa kufuga ni kuboresha uzalishaji na kuendeleza kizazi bora. Kuna aina nyingi za mbuzi/kondoo wanaoweza kufugwa kulingana na mazingira na mahitaji ya mfugaji. Uchaguzi hufanyika kwa kuangalia umbile, uzalishaji na kumbukumbu za wazazi kama vile umbo kubwa, ukuaji wa haraka, uwezo wa kutunza vitoto na kutoa maziwa mengi.
Mbuzi/kondoo jike wanaofaa kwa ajili ya kuzalisha maziwa na nyama wawe na sifa zifuatazo:-
- Historia ya kukua upesi, kuzaa (ikiwezekana mapacha) na kutunza vitoto vizuri,
- Umbo la mstatili linaloashiria utoaji wa nyama nyingi; na
- Asiwe na ulemavu wa aina yoyote
- Awe na miguu ya nyuma iliyo imara na iliyonyooka na yenye nafasi kwa ajili ya kiwele; na
- Awe na kiwele kikubwa na chuchu ndefu zilizokaa vizuri
Dume bora awe na sifa zifuatazo:-
- Miguu iliyonyooka, imara na yenye nguvu,
- Asiwe na ulemavu wa aina yoyote,
- Mwenye uwezo na nguvu ya kupanda; na
- Mwenye kokwa mbili zilizo kaa vizuri na zinazolingana
Utunzaji huanza mara tu baada ya kuzaliwa. Mfugaji ahakikishe:-
- Kitoto cha mbuzi/kondoo kinapata maziwa ya mwanzo (dang’a) ndani ya masaa 24 tangu kuzaliwa na kwa muda wa siku 3,
- Kama kinanyweshwa maziwa, kipewe lita 0.7- 0.9 kwa siku. Maziwa haya, ni muhimu kwani yana viinilishe na kinga dhidi ya magonjwa,
- Iwapo mama hatoi maziwa au amekufa, inashauriwa kutengeneza dang’a mbadala au kama kuna mbuzi/kondoo mwingine aliyezaa anaweza kusaidia kukinyonyesha kitoto hicho,
- Kitoto cha mbuzi/kondoo kiendelee kunyonya kwa wiki 12 - 16. Wiki 2 baada ya kuzaliwa, pamoja na maziwa, kianze kupewa vyakula vingine kama nyasi laini na chakula cha ziada ili kusaidia kukua kwa tumbo. Aidha, kipewe maji wakati wote,
- Vyombo vinavyotumika kulishia vinakuwa safi muda wote,
- Kitoto cha mbuzi/kondoo kiachishwe kunyonya kikiwa na umri wa miezi 3 hadi 4 kutegemea afya yake; na
- Vitoto vipatiwe kinga na tiba ya magonjwa kulingana na ushauri wa mtaalam wa mifugo.
Utambuzi
Mbuzi huwekewa alama ili atambulike kwa urahisi na kuwezesha utunzaji wa kumbukumbu zake. Shughuli hii hufanyika kwa mbuzi/kondoo akiwa na umri wa siku 3 - 14. Njia zitumikazo ni pamoja na:
- Kuweka alama sikioni kwa kukata sehemu ndogo ya sikio,
- Kumpa jina kwa wafugaji wenye mbuzi wachache,
- Kumvisha hereni ya chuma au plastiki yenye namba kwenye sikio,
- Kumvalisha mkanda wenye namba shingoni; na
- Kuweka namba kwa kuunguza sehemu ya ngozi ya mbuzi. Pale mfugaji anapotumia njia hii inashauriwa aweke alama kwenye eneo ambalo halitaathiri ubora wa ngozi
Mbuzi/kondoo aondolewe vishina vya pembe akiwa na umri kati ya siku 3 hadi 14.
Visipoondelewa hukua na kusababisha kuumizana na kuhitaji nafasi kubwa kwenye banda. Kazi hii ifanywe na mtaalam wa mifugo.
Kuhasi
Vitoto vya mbuzi/kondoo ambavyo havitatumika kwa ajili ya kuendeleza kizazi vihasiwe kabla ya kufikia umri wa miezi 3. Kazi hii ifanywe na mtaalam wa mifugo.
Utunzaji wa Mbuzi/Kondoo wa Miezi 4 - 8
Mbuzi wa miezi 4 mpaka 8 ni wale ambao wameacha kunyonya mpaka umri wa kupandishwa kwa mara ya kwanza. Mbuzi wa umri huu wana uwezo wa kula aina mbalimbali za malisho kama nyasi, mikunde, miti malisho na mabaki ya mazao wakati kondoo hupendelea zaidi nyasi fupi. Wakati wa kiangazi huhitaji kupatiwa chakula cha ziada au kupewa pumba za nafaka mbalimbali, mashudu ya alizeti, pamba na dengu, majani ya mikunde yaliyokaushwa, madini na vitamini.
Katika ufugaji huria ni vema kuzingatia idadi ya mbuzi/kondoo inayoweza kuchungwa katika eneo, aina na hali ya malisho.
Ili mbuzi/kondoo aweze kukua na kufikia uzito wa kuchinjwa/kupevuka mapema, mfugaji anapaswa kufuata kanuni za ufugaji bora zifuatazo:-
- Kumpatia vyakula vya ziada kwa muda wa miezi 2 mfululizo kiasi cha kilo 0.2 – 0.7 kwa siku kuanzia anapoachishwa kunyonya,
- Kumpatia dawa ya kuzuia minyoo kila baada ya miezi 3 na kutoa kinga za magonjwa mengine kama itakavyoshauriwa na mtaalam wa mifugo,
- Kuchanja na kuogesha ili kuzuia magonjwa mbalimbali,
- Kukata kwato mara zinapokuwa ndefu; na
- Kuhasi madume yasiyotumika kuzalisha.
Mbuzi/kondoo wakitunzwa vizuri wanaweza kupandishwa wakiwa na umri wa miezi 8 hadi 12 kwa mbuzi/kondoo walioboreshwa na miezi 18 hadi 24 kwa mbuzi wa asili kutegemea afya yake. Hata hivyo, inashauriwa wapandishwe wanapofikia uzito wa kilo 12 au zaidi na wasipandishwe mbuzi/kondoo wa ukoo mmoja.
Dalili za joto
Mfugaji anashauriwa asimpandishe jike kabla hajafikisha umri wa kupandwa wa miezi 8 hadi 12 kwa mbuzi/kondoo walioboreshwa na miezi 18 hadi 24 kwa mbuzi wa asili hata kama ataonyesha dalili ya kuhitaji dume. Mbuzi/kondoo aliyezaa anaweza kupandishwa siku 30-60 baada ya kuzaa. Mbuzi/kondoo aliyeko kwenye joto huonyesha dalili zifuatazo:-
- Hutingisha/huchezesha mkia,
- Hupanda na kukubali kupandwa na wengine,
- Hutoa ute mweupe ukeni,
- Huhangaika mara kwa mara na kupiga kelele,
- Hufuata madume,
- Hamu ya kula hupungua,
- Hukojoa mara kwa mara,
- Uke huvimba na huwa mwekundu kuliko ilivyo kawaida; na
- Kwa mbuzi anayekamuliwa hupunguza kiwango cha maziwa
Utunzaji wa Mbuzi/Kondoo Mwenye Mimba
Kwa kawaida mbuzi/kondoo hubeba mimba kwa muda wa miezi 5. Utunzaji wambuzi/kondoo mwenye mimba ni muhimu kwani ndiyo chanzo cha kupata vitoto vyenye afya bora. Mfugaji anashauriwa kufuata kanuni zifuatazo:
- Apatiwe vyakula vya ziada kilo 0.2 – 0.7 kwa siku ili kutosheleza mahitaji yake na kitoto kinachokua tumboni,
- Apatiwe nyasi, miti malisho na mikunde mchanganyiko kilo 1.8 – 2.5 kwa siku.
- Huhangaika kwa kulala na kuamka mara kwa mara,
- Sehemu ya nje ya uke hulegea,
- Hujitenga na kundi na hutafuta sehemu kavu na yenye kivuli,
- Hupiga kelele; na
- Hutokwa na ute mzito ukeni.
Utunzaji wa Mbuzi/Kondoo Anayenyonyesha
Mbuzi/kondoo anayenyonyesha huhitaji chakula kingi zaidi ili kukidhi mahitaji ya mwili na kuzalisha maziwa kwa ajili ya kitoto/vitoto. Pamoja na nyasi, mikunde na majani ya miti malisho kilo 1.8 – 2.5 kwa siku ni muhimu apewe chakula cha nyongeza kilo 0.3 – 0.8 kwa kila lita ya maziwa inayoongezeka baada ya lita 2 na maji safi, salama na ya kutosha wakati wote.
Taratibu za Kuzingatia Katika Ukamuaji wa Mbuzi wa Maziwa
Lengo la ufugaji wa mbuzi/kondoo wa maziwa ni kupata maziwa mengi, safi nasalama pamoja na mazao yatokanayo na maziwa. Mambo muhimu ya kuzingatia ni:-
- Sehemu ya kukamulia iwe safi na yenye utulivu,
- Mbuzi/kondoo awe na afya nzuri, msafi, na kiwele kioshwe kwa maji safi ya uvuguvugu,
- Mkamuaji asibadilishwe badilishwe awe msafi, mwenye kucha fupi na asiwe na magonjwa ya kuambukiza,
- Vyombo vya kukamulia viwe safi; na
- Maziwa ya mwanzo kutoka kila chuchu yakamuliwe kwenye chombo maalum (strip cup) ili kuchunguza ugonjwa wa kiwele.
Dume bora la mbegu ni muhimu litunzwe ili liwe na uwezo wa kutoa mbegu bora, kupanda na kuzalisha. Dume bora huanza kupanda akiwa na umri kati ya miezi.8 - 10 kwa mbuzi walioboreshwa. Katika msimu wa kupandisha dume moja liruhusiwe kupanda majike 40 hadi 50. Aidha, inashauriwa madume wenye umri wa miezi 8 – 9 waruhusiwe kupanda majike ambao ndio mara ya kwanza kupandwa.
Dume apatiwe:-
- Malisho ya kutosha na vyakula vya ziada kiasi kisichopungua kilo 0.2 – 0.7
- kwa siku na maji ya kutosha,
- Majani ya miti malisho, mikunde na nyasi mchanganyiko na mabaki ya mazao; na
- Kilo 0.45 hadi 0.9 za chakula cha ziada za nyongeza kwa siku kulingana na uzito wake na wingi wa majike anayopanda.wiki 2 kabla na baada ya kuanza kupanda.
Kukata Mkia
Mara nyingine kondoo hukatwa mkia ili kuruhusu mtawanyiko mzuri wa mafuta katika misuli mwilini. Pia kondoo aliyekatwa mkia huwa msafi. Kazi hii ifanywe kama itakavyoshauriwa na mtaalam wa mifugo kwa kutumia vyombo maalum. Inashauriwa mkia ukatwe urefu wa sentimita 2.5 – 3.8 kutoka kwenye shina la mkia wakati kondoo akiwa na umri wa siku 3 mpaka mwezi 1.
Kumnyoa Kondoo wa Sufu
Sufu hunyolewa wakati kondoo akiwa hai au amechinjwa. Kwa kawaida hunyolewa miezi 6 hadi mwaka 1 ambapo sufu huwa imefikia urefu wa sentimita 15 – 20. Vifaa vinavyotumika ni pamoja na mikasi au visu maalum. Uangalifu unahitajika wakati wa kunyoa ili ngozi ya kondoo isiharibike. Unyoaji ufanyike wakati wa kiangazi na siyo wakati wa mvua, kondoo akiwa na mimba au kipindi cha majani kutoa mbegu.
Udhibiti wa Magonjwa ya Mbuzi na Kondoo
Magonjwa husababishwa na vimelea jamii ya virusi, bakteria, protozoa na riketsia.
Magonjwa mengine husababishwa na upungufu wa viinilishe, vitamini na protini.
Dalili za mbuzi/kondoo mgonjwa ni pamoja na:-
- Manyoya husimama,
- Kuzubaa, kusinzia, kukohoa na kupiga chafya,
- Kukosa hamu ya kula na kunywa maji,
- Kujitenga na kundi,
- Kuvimba taya la chini,
- Kupumua kwa shida,
- Kutokwa na machozi na makamasi,
- Kuwa na upele au uvimbe kwenye sehemu ya mwili; na
- Kutupa mimba.
Chanjo na kinga
- Mbuzi na kondoo wachanjwe dhidi ya magonjwa ya homa ya maapafu. Ugonjwa huu ni hatari sana na huenea kwa njia ya hewa na unaweza kusababisha vifo kati ya asilimia 60-100,
- Kila baada ya miezi 6 mifugo ipatiwe kinga dhidi ya ugonjwa wa miguu na midomo na magonjwa mengine kama Kimeta, bonde la ufa, kutupa mimba na chambavu (BQ) zitolewe kulingana na ushauri wa mtalaam wa mifugo,
- Kama kuna wanyama walioathirika watengwe kwenye kundi, wasisafirishwe au kuuzwa,
- Mbuzi/kondoo wapatiwe dawa ya minyoo. Vitoto vya mbuzi/kondoo vipatiwe dawa ya minyoo vinapofikia umri wa mwezi 1. viendelee kupatiwa dawa ya minyoo kila mwezi hadi vinapofikia miezi 5 na baada ya hapo vipatiwe dawa ya minyoo kila baada ya miezi 3 - 4; na
- Zingatia usafi wa banda ili kuwakinga na ugonjwa wa kuharisha na kuharisha damu na magonjwa mbalimbali.
Kuweka kumbukumbu za mifugo ni muhimu katika uzalishaji kwa ajili ya kutambua kosaafu, gharama za utunzaji na faida. Pia, humsadia mfugaji kufanya maamuzi katika uendelezaji wa ufugaji wake. Mtalaamu wa mifugo pia anaweza kutumia kumbukumbu hizi ili kumsaidia mfugaji kuboresha ufugaji wake.
Kumbukumbu muhimu zinazohitajika kutunzwa ni:-
- Kumbukumbu za idadi na ukuaji wa wanyama waliopo, jinsi zao, uzito wa mbuzi/kondoo kwa kila mwezi ili kufuatilia ukuaji wake, tarehe ya kuachishwa kunyonya na idadi ya waliouzwa,
- Kumbukumbu ya uzazi zinazoonyesha tarehe ya kuzaliwa, namba yake, jinsi yake, aina (breed), namba ya dume/jike, na uzito wa kuzaliwa,
- Kumbukumbu za upandishaji zinazoonyesha namba ya mbuzi/kondoo anayepandwa, tarehe ya joto na ya kupandwa, namba ya dume lililotumika kupanda, tarehe ya joto la pili kama atarudia na tarehe ya kuzaa,
- Kumbukumbu za chanjo na matibabu zinazoonyesha namba ya mbuzi/kondoo, tarehe ya matibabu, aina ya chanjo au ugonjwa, dawa iliyotumika, idadi ya waliokufa na waliopona na jina la mtaalam aliyetibu,
- Kumbukumbu za maziwa zinazoonyesha namba ya mbuzi/kondoo, tarehe ya kuzaa, kiasi cha maziwa kwa siku, na kiasi cha maziwa kwa kipindi chote cha kukamuliwa, tarehe ya kuacha kukamua na idadi ya siku alizokamuliwa,
- Kumbukumbu za mapato na matumizi zinazoonyesha mapato na matumizi, vitu vilivyouzwa au kununuliwa kwa siku, kiasi cha fedha unachokuwa nacho kila wakati, kiasi cha fedha unachodai na kudaiwa.
Comments
Post a Comment