Skip to main content

Mambo Muhimu Ya Kuzingatia Katika Utayarishaji Wa Mihogo Mibichi Na Ukaushaji



Utayarishaji
  • Mihogo mibichi iliyovunwa huoshwa mara mbili. Uoshaji wa kwanza ni ule wa kuondoa udongo baada ya kuvuna, na uoshaji wa pili ni baada ya kumenya mihogo kabla ya kukausha.
  • Baada ya kuoshwa mihogo humenywa kwa kutumia kisu kikali, na kutumbukizwa ndani ya maji safi. Baada ya kumenya kiasi kinachotakiwa mihogo huoshwa na maji safi hadi kuwa myeupe.
Utengenezaji wa chipsi
Mihogo iliyo safi huwekwa ndani ya mashine ya kuzungushwa kwa mikono au mashine ya kuzungushwa kwa mota ya umeme, kisha huparuliwa na kutoka vipande vidogo vidogo ambavyo huanikwa katika makaushio bora.
Kwa mihogo michungu
Baada ya kuparuwa mihogo kuwa chipsi, huwekwa katika mifuko safi (viroba) na kuwekwa mahali penye kivuli kwa muda usiopungua saa sita ili kuacha sumu iliyoko kwenye mihogo kupotea kabla ya kukausha.
Ukaushaji
  • Mihogo safi ambayo imeparuliwa au kukatwa vipande vidogo vidogo hukaushwa katika makaushio bora kwenye jua kali. Makaushio bora huwa ni yale ambayo yamejengewa kichanja kilichoinuliwa mita mbili kutoka ardhini, na kutandazwa chekeche ya plastiki juu yake, yenye matundu madogo yasiyoweza kupitisha chembechembe za mihogo mikavu Kitambaa safi cha kaniki au mikeka safi huweza kutumika pia kama tandiko la juu ya kichanja ambapo chipsi za mihogo huweza kukaushwa kwa hali ya usafi.
  • Epuka kukaushia chipsi za mihogo katika majamvi mabovu juu ya ardhi kwani uchafu utakaoingia ndani ya mihogo hautakuwa rahisi kuondoa tena na husababishsa bidhaa ya unga kutokuwa na ubora.
Ukaushaji duni wa mihogo
Uharibifu au upotevu unaosababishwa na ukaushaji duni [wa kienyeji]unatokana na muhogo kubadilika rangi na na kupata ukungu.
Njia bora za kukausha mihogo
Mihogo iliyoparuliwa (chipsi) hukaushwa na baadaye kusindikwa ilikupata unga.

Vifaa na malighafi
  • Mihogo safi
  • Kisu kikali kisichoshika kutu.
  • Mashine ya kuparua (grater)
  • Kaushio bora
  • Kitambaa cheusi kikubwa cha kutosha na kilicho safi au majamvi safi
  • Vifungashio.
Utengenezaji wa makopa ya mihogo
  • Menya mihogo safi kuondoa maganda
  • Parua kwa kutumia mashine kupata chipsi.
  • Anika kwenye kichanja au kaushio bora lilotandikwa kitambaa cheusi kilicho safi au jamvi safi ili kuzuia uchafu kuingia ndani ya chipsi.
  • Sambaza na geuzageuza vipande hivyo ili kuharakisha ukaukaji.
  • Muda wa kukausha hutegemea hali ya jua na ukubwa wa vipande. Vipande vidogo hukauka upesi na huwa bora kwa mlaji. Vipande vikubwa huchelewakukauka na hupoteza ubora
  • Fungasha vipande vilivyokaushwa kwenye magunia safi, kisha hifadhi kwenye maghala bora.
Hifadhi ya Mihogo Mikavu (Chipsi Au Makopa)
  • Njia pekee ya kuhifadhi mihogo kwa muda mrefu ni kwa kuhifadhi mihogo iliyokaushwa. Muhogo uliokaushwa huweza kuhifadhiwa kwa muda wa miezi 6 hadi 12 bila kuharibika.
  • Makopa yanashambuliwa na dumuzi zaidi kuliko chipsi , hivyo inashauriwa kuhifadhi mihogo iliyoparuliwa na kukaushwa (chipsi) ambayo inakuwa katika hali ya unga unga na kufanya mashambulizi ya dumuzi yapungue kabisa.
  • Chipsi za mihogo zinaweza kuhifadhiwa katika magunia safi ya juti na kupangwa ndani ya ghala juu ya chaga. Pia chipsi zinaweza kuhifadhiwa katika hali ya kichele ndani ya sailo au kihenge bora. Mihogo haihifadhiwi kwa kutumia madawa ya viwandani. Hifadhi kwa hali ya ukavu, usafi na kagua ghala mara kwa mara kuona kama kuna mashambulizi ya panya na chukua tahadhari kuepuka upotevu wa chakula hicho. Aidha hifadhi kwa muda ulioshauriwa ili kudumisha ubora wa bidhaa.
Kusindika muhogo uliokaushwa kupata unga
Vifaa
  • Mashine ya kusaga
  • Mifuko ya kufungasha
  • Mashine ya kufungia mifuko
  • Chekeche
Jinsi ya kusindika
  • Saga muhogo uliokaushwa kwenye mashine ili kupata unga.
  • Chekecha kwa kutumia chekeche laini. Ukubwa wa matundu ya chekechekeche hutegemea kiwango cha ubora wa unga kinachotakiwa na soko.
  • Weka unga kwenye mifuko kutegemea matakwa ya soko (kilo 1,2,5,10, au 50)
  • Funga vyema kwenye mifuko ya kufungashia ili hewa isiingie
  • Hifadhi kwenye chaga au fremu zilizowekwa mahali pakavu na pasipokuwa na mwanga mkali.
Viwango vya ubora wa unga wa muhogo uliokaushwa
Unga laini
Unga huu unapochekechwa kwa kutumia chekeche yenye matundu madogo (milimita 0.60) hupenya karibu wote (asilimia 90)
Unga wenye ulaini kati
Unga huu unapochekechwa kwa kutumia chekeche yenye matundu makubwa (milimita) 1.20) hupenya karibu wote (asilimia 90).
Matumizi ya Unga wa Muhogo
Hutumika kupika ugali, uji na katika kutengeneza maandazi, tambi, keki, biskuti, kababu, donati, mkate, chapati na chapati maji.

Comments

Popular posts from this blog

Utengenezaji wa Chakula cha Kuku wa Nyama (Bloilers)

Utangulizi Kuku wa nyama wana mahitaji yafuatayo ya viinilishe katika chakula ili wakue vizuri Viinilisha vya wanga 60-65%   Protini 30-35%   Madini 2-8% Chakula cha Vifaranga Chakula hiki hutengenezwa katika namna ya kumsaidia kifaranga aweze kumeza vizuri na hivyo hakitakiwi kuwa katika punje punje. Hata kama utanunua pumba, ni vema kuzipitisha kwenye mashine ili ziwe laini zaidi.  Mahitaji (kgs)  Unga wa dona wa nafaka kama mahindi au mtama 40  Pumba za mtama au mahindi au uwele 27  Mashudu ya alizeti au ufuta, au pamba au karanga n.k. 20  Unga wa mifupa au chokaa ya kuku (DCP) 2.25  Dagaa au mabaki ya samaki (sangara fish meal) 10  Chumvi ya jikoni 0.5  Virutubisho (Broiler premix) 0.25  Jumla utapata 100Kg. Chakula cha kukuzia – growers mash Mahitaji (Kg) Mahindi yaliyobarazwa au mtama au uwele 25   Pumba za mtama au mahindi au uwele 44   Mashudu ya alizeti au ufuta, au pamba au karanga n.k. 17   Unga wa mifupa a...

Aina Za Miti ya Minazi

AINA ZA MINAZI Inafaa mkulima kufahamu kuna aina mbali mbali za minazi na ina mahitaji tofauti katika ukuaji. Ujuzi huu utamsaidia katika kuchagua aina ya minazi itakayofaa kwa eneo lake na kwa kiwango chake cha utunzaji. KUNA AINA TATU ZA MINAZI Minazi mirefu ya asili Minazi mifupi Minazi chotara MINAZI MIREFU YA ASILI (EAT) Minazi ya aina hii ndiyo inayojulikana na wakulima wengi kwa vile ni ya kiasili na imezoea mazingira yetu. Minazi hii huchukua miaka 6-8 tangu kupandikizwa hadi kuzaa. Minazi ya aina hii huvumilia ukame na inao uwezo wa kutoa wastani wa nazi 40 kwa mwaka. Nazi huwa kubwa na zenye nyama nene ambayo inafaa kwa kupikia na kukamua mafuta. Minazi hii huishi kad ya miaka 60 na kuendelea. Nchini Tanzania, minazi hii hustawi vyema ukanda wa pwani sehemu zisizo na mawe na ambazo hazituamishi maji. MINAZI MIFUPI (DWARF) Minazi ya aina hii huzaa mapema kuanzia miaka miwili. Huzaa nazi nyingi na ndogo. Nazi hizi huwa na nyama nyembamba hivyo hutumika kwa nnadafu. Minazi huhit...

Kilimo Bora cha Migomba

UTANGULIZI Hapa Tanzania kilimo cha migomba kimekuwepo Kwa miaka mingi. Kilimo hiki ni maarufu sana kwa sababu zao la ndizi limekuwa likitumika kama chakula kikuu kwa baadhi ya mikoa kama vile Kagera, Kilimanjaro na Mbeya na hivyo kulifanya muhimu, kufuatia mazao ya mahindi, mpunga, mtama, muhogo,viazi na mazao ya jamii ya kunde kama vile maharage. Zao la ndizi linaweza kuwa moja kati ya mazao ya biashara iwapo litazalishwa kwa kufuata kanuni bora za uzalishaji wa zao hilo, ikwa ni pamoja na kupanda aina bora ya migomba inayozaa ndizi zinazotambulika katika masoko ya kimataifa. ASILI YA MIGOMBA Asili ya migomba ni nchi za Malaysia na India ambazo ziko Kusini Mashariki mwa Asia. Migomba inayolimwa sasa imetokana na migomba ijulikanayo kama Musa balbisiana ambayo asili yake ni India, na Musa acuminata ambayo asili yake ni Malaysia. Kutoka Malaysia na India migomba ilifika Afrika Mashariki katika karne ya tano MAENEO YANAYOLIMWA MIGOMBA NCHINI Nchini Tanzania mikoa inayoshughulika na kili...